Jun 24, 2022 07:47 UTC
  • UNICEF: Watoto milioni 8 hatarini kufariki dunia kutokana na uzito mdogo

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF limeonya kuwa, takriban watoto milioni nane walio na umri wa chini ya miaka mitano katika nchi 15 zinazokabiliwa na majanga wako katika hatari ya kifo kutokana na uzito mdogo kupindukia endapo hawatapata haraka matibabu ya lishe na huduma zinazotakiwa.

Indhari hiyo imetolewa mjini Geneva Uswisi wakati viongozi wa dunia kutoka nchi saba tajiri zaidi duniani au G7 wakijiandaa kwa mkutano wao.

Kwa mujibu wa UNICEF, idadi ya watoto walioathirika inaongezeka kila dakika na tangu kuanza kwa mwaka huu, kuongezeka kwa mgogoro wa chakula duniani kumesababisha watoto 260,000 zaidi au mtoto mmoja kila sekunde 60 kuteseka kutokana na uzito mdogo kupindukia katika nchi 15 zinazobeba mzigo mkubwa wa mgogoro huo, ikiwa ni pamoja na mataifa katika Pembe ya Afrika na Sahel ya kati.  

Ongezeko hilo la upotevu mkubwa wa uzito kupindukia ni pamoja na viwango vilivyopo vya utapiamlo wa watoto ambavyo UNICEF mwezi uliopita ilionya kuwa umefurutu ada. 

Catherine Russell

Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Catherine Russell amesema “Hivi sasa tunashuhudia hali mbaya sana ya viwango vya watoto kupoteza uzito kupindukia na ni hali inayoonghezeka kwa kasi. Hivyo msaada wa chakula ni muhimu, lakini hatuwezi kuokoa watoto wenye njaa na mifuko ya ngano. Tunahitaji kuwafikia watoto hawa sasa na matibabu muhimu kabla hatujachelewa.” 

UNICEF imesema mifumo dhaifu ya kinga huongeza hatari ya kifo kati ya watoto chini ya miaka mitano hadi mara 11 ikilinganishwa na watoto walio na lishe bora.../ 

Tags