Ulaya yalegeza msimamo katika vikwazo vya mafuta ilivyoiwekea Russia
(last modified Sun, 26 Jun 2022 02:28:06 GMT )
Jun 26, 2022 02:28 UTC
  • Ulaya yalegeza msimamo katika vikwazo vya mafuta ilivyoiwekea Russia

Shirika la habari za uchumi la Bloomberg limeripoti kuwa, ukiwa haujatimia hata mwezi mmoja tangu Umoja wa Ulaya ulipoiwekea Russia vikwazo vya mafuta, bara hilo limeongeza kiwango cha mafuta linachonunua kwa Moscow.

Mwanzoni mwa mwezi huu wa Juni, Umoja wa UIaya EU ulipitisha marufuku ya kununua kiwango fulani cha mafuta kutoka Russia na kujipangia kwamba, hadi ifikapo mwaka ujao itasitisha ununuzi wa hadi asilimia 90 ya mafuta ya nchi hiyo.

Marufuku hiyo imehusisha mafuta yote yanayosafirishwa kwa njia ya bahari kwa kutumia meli lakini ikatoa msamaha kwa mafuta yanayosafirishwa kwa kutumia mabomba.

Ripoti ya Jumamosi ya Bloomberg imenukuu takwimu za vituo vya baharini vya ufuatiliaji wa meli za mafuta na kuonyesha kuwa, katika wiki iliyopita, viwanda vya usafishaji mafuta vya Ulaya vilinunua kwa siku mapipa milioni moja, laki nane na elfu arubaini ya mafuta, likiwa ni ongezeko la wiki ya tatu mtawalia na kiwango cha juu zaidi cha mafuta ambayo Ulaya, ikijumuishwa na Uturuki, zimepokea kutoka Russia katika muda wa karibu miezi miwili sasa.

Mnamo mwanzoni mwa mwezi huu, jarida la Economist liliripoti kuwa, licha ya ahadi uliyojiwekea Umoja wa Ulaya ya kupunguza uagizaji mafuta kutoka Russia, uuzaji wa mafuta ya nchi hiyo kwa EU katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Aprili umeongezeka kwa asilimia 14.../

Tags