Kukataa India ombi la Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i85934-kukataa_india_ombi_la_marekani
India imekataa ombi la Marekani ambayo iliitaka nchi hiyo iziwekee vikwazo meli za Russia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 16, 2022 08:34 UTC
  • Kukataa India ombi la Marekani

India imekataa ombi la Marekani ambayo iliitaka nchi hiyo iziwekee vikwazo meli za Russia.

Serikali ya India imekuwa ikijaribu kudhihirisha msimamo huru katika mvutano kati ya Marekani na Russia huku ikisisitiza juu ya haki yake ya kuchagua washirika wake wa kimataifa na kuamiliana nao ili kudhamini maslahi yake ya kitaifa, na hivyo imekataa ombi la Marekani ambayo iliitaka New Delhi izizuie meli za Russia kuingia katika bandari ya Mumbai. Serikali ya Marekani katika miaka ya karibuni imefanya juhudi kubwa ili kuunda muungano wa kikanda ikiwa ni pamoja na kuishirikisha India katika muungano huo dhidi ya China na Russia.  

Meli ya Russia katika bandari ya Mumbai, India 

Wakati huo huo serikali ya New Delhi hadi sasa haiko tayari kushirikiana na Marekani dhidi ya Moscow; kwani India ina uhusiano wa kistratejia na Russia. Ni wazi kuwa kwa upande wa China pia kutokana na kuwa kwake jirani na India inatekeleza kwa tahadhari sera zake dhidi ya Beijing katika kalibu ya ushirikiano wake na Marekani. 

Susan Sharma mchambuzi wa masuala ya India anazungumzia hili akisema: Washington inajaribu kila linalowezekana kuivuta India katika miungano yake ili kuitumia nchi hiyo kukabiliana na satwa ya China na pia Russia. Hii ni katika hali ambayo India pia inafuatilia kwa makini malengo na maslahi yake nje ya mashinikizo ya kikanda na kimataifa katika bahari ya Hindi na kusini mashariki mwa Asia.  

India imekuwa na uhusiano wa kistratejia na Moscow tangu zama za Umoja wa Kisovieti; na moja ya daghadagha zinazoisibu Marekani siku zote pia ni hii ya kutaka kuhitimisha ushirikiano huo wa pande mbili. Kuhusiana na suala hilo, Washington inafanya kila linalowezekana kwa kutoa baadhi ya fursa kwa New Delhi ikiwemo kuondoa vikwazo vya kijeshi ili kuishawishi ijitoe katika kambi ya Moscow na kujiunga na mhimili wa sera za Washington. Hii ni katika hali ambayo, Russia inaendelea kuwa sehemu muhimu ya mipango na mfumo wa kijeshi wa India; huku New Delhi ikifuatilia kustawisha uhusiano kati yake na Kremlin pia ili kuzuia ushirikiano wa kimkakati kati ya Moscow na Islamabad ambayo ni hasimu wa nyuklia wa India. 

Uhusiano wa kimkakati kati ya India na Russia 

Geeta Kochhar, Profesa katika Chuo Kikuu cha Jawajarlal Nehru anasema: India haihitaji kushirikiana na Marekani kwa ajili ya kuweka sawa siasa zake za kikanda. Hii ni kwa sababu, chini ya fremu ya siasa zake zisizoegemea upande wowote, New Delhi haishirikiani na dola lolote kwa ajili ya kuliangamiza dola jingine.

Ala kulli hal, hatua ya India ya kupinga maombi ya Marekani kuhusu Russia haiishii katika kukataa kwake ombi la Marekani la kuiwekea Russia vikwazo bali hivi karibuni New Delhi ilikataa pia ombi la Washington ambayo iliitaka nchi hiyo isinunue mafuta kutoka Russia. Marekani sasa inahaha huku na kule baada ya kuibuka mgogoro wa Ukraine ili kuasisi muungano dhidi ya Russia na hivyo kupelekea nchi hiyo kutengwa; jitihada ambazo hata hivyo zimegonga mwamba. Hii ni kwa sababu nchi mbalimbali hasa India zinaainisha sera zao za kikanda na kimataifa kwa mujibu wa maslahi yao ya kitaifa; na ndio maana sera za Washington za kuipinga Russia kikanda na kimataifa zimefeli.