Kuendelea mgogoro wa nishati barani Ulaya
(last modified Wed, 14 Sep 2022 02:11:35 GMT )
Sep 14, 2022 02:11 UTC
  • Kuendelea mgogoro wa nishati barani Ulaya

Nchi za Ulaya ambazo kwa sasa zinakabiliwa na tatizo kubwa la kusambaza gesi na kudhibiti bei ya nishati, zinakumbwa na changamoto mbalimbali za kisiasa na kijamii zinazotokana na tatizo hilo.

Baadhi ya serikali za Ulaya pia zimetaka kusitishwa mara moja siasa za kuwekewa vikwazo sekta ya mafuta na gesi ya Russia. Kuhusiana na suala hilo, Kyriakas Mitsotakis Waziri Mkuu wa Ugiriki, amesema kuwa vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Russia vimerejea Ulaya kwenyewe na kuharibu uchumi wa nchi za bara hilo.

Kushadidishwa vikwazo vya Ulaya dhidi ya Russia, ambavyo vinatekelezwa kwa mujibu wa siasa za Marekani kuhusu vita vya Ukraine; kwa miezi kadhaa sasa kumepelekea kupunguzwa au kusimamishwa kabisa mtiririko wa gesi ya Russia kwenda nchi za Ulaya. Hali hiyo imeathiri sana uchumi wa nchi hizo, hasa zile zilizo na nguvu kubwa za kiuchumi kama Ujerumani. Kwa hakika, ukosefu wa gesi umesababisha kuongezeka pakubwa bei ya mafuta na kuongeza sana gharama ya uzalishaji umeme na bidhaa pamoja na huduma muhimu huko Ulaya, ambapo baadhi ya viwanda ama vimefilisika au viko njiani kusambaratika.

Nchi za Ulaya ziliyawekea vikwazo mafuta na gesi ya Russia kwa uchochezi wa Marekani

Hali hiyo imekuwa changamoto kubwa kwa nchi dhaifu za Ulaya kama vile Ugiriki, Italia na za Ulaya Mashariki. Kama alivyokiri Waziri Mkuu wa Ugiriki, nchi za Ulaya Magharibi licha ya kuelewa matokeo mabaya ya vikwazo vya nchi hizo dhidi ya Russia, lakini hazina nia ya kubadilisha mikakati yao dhidi ya nchi hiyo.

Bila shaka nchi za Ulaya hazina budi ila kufuata siasa za Washington kuhusu vita vya Russia na Ukraine. Kwa kweli, vita vya sasa Ukraine ni vita vya nishati kati ya Marekani na Russia, ambavyo vinafanyika katika ardhi ya Ulaya. Hii ni katika hali ambayo Marekani, kutokana na kunufaika na rasilimali za mafuta na gesi, sio tu kwamba haitatiziki na vita hivyo, bali pia inapata faida kubwa kwa kuongeza mapato yanayotokana na mauzo ya mafuta na gesi nje ya nchi. Russia, kwa kutafuta wateja wapya wa Asia na kuongeza mauzo ya gesi kutoka nchi kama vile Uchina, imeweza kufidia kwa kiasi kikubwa uharibifu uliosababishwa na nchi za Magharibi katika sekta yake ya nishati. Wakati huo huo, kutokana na kuongezeka bei ya mafuta na gesi duniani, mapato ya Russia pia yameongezeka.

Vladimir Ivin, Mkuu wa Idara ya Huduma za Forodha ya Shirikisho la Russia, anasema kuhusu suala hilo kwamba: Mapato ya dola ya Russia yanayotokana na mauzo ya mafuta na gesi yameongezeka mara 1.5.

Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa, Russia ilipata dola bilioni 158 kutokana na mauzo ya nje ya nishati katika miezi sita baada ya kuanza vita vya Ukraine.

Hii ni katika hali ambayo nchi za Ulaya zina wasiwasi mkubwa wa kukabiliwa na hali ngumu katika majira ya baridi kali yanayokuja, na hitilafu zinazidi kuongezeka siku baada ya nyingine kati ya wanachama wa Umoja wa Ulaya. Kwa mfano, Miklas Beck, Waziri wa Masuala ya Ulaya wa Jamhuri ya Czech, ameonya kwamba msimamo wa ukosoaji wa Budapest kuhusu vikwazo vya Russia utaifanya Hungary kuondokewa katika Umoja wa Ulaya.

Viktor Orban, Waziri Mkuu wa Hungary ameweza kudhibiti mzozo wa nishati wa nchi yake kwa kukataa kutekeleza vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya dhidi ya mafuta na gesi ya Russia. Kuhusiana na hilo, ameonya kuwa maelfu ya vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi dhidi ya Russia havijafaulu kufikia malengo yaliyokusudiwa na badala yake vimeitumbukiza Ulaya katika mgogoro mkubwa wa nishati.

Viktor Orban

Huku msimu wa baridi kali ukikaribia barani Ulaya, mgogoro wa kudhamini nishati barani humo umefikia kiwango hatari zaidi. Kwa sasa nchi za Ulaya zimenasa kati ya machaguo mawili ya kutekeleza au kutotekeleza siasa na matakwa ya Washington kuhusu vita vya Ukraine, na kwa upande mwingine, kuendelea siasa hizo za uhasama kunazidisha tu migogoro ya kisiasa na kijamii ya Umoja wa Ulaya na wakati huo huo kuibuia mivutano kati ya wanachama wake.

Chuo cha Carnegie chenye makao makuu yake mjini Washington nchini Marekani kinasema kuhusu suala hili kwamba: Haya hayatakuwa tu majira yenye baridi kali kwa Ulaya, bali bara hilo linapasa kujiandaa kukabiliana na hali hiyo ngumu kwa miaka miwili au mitatu hivi. Kwa upande mwingine, kuna uwezekano mkubwa kwamba Ulaya haitapata chanzo kingine kikuu mbadala cha kujidhaminia gesi katika soko la dunia hadi mwaka 2025.

Tags