Maandamano dhidi ya ufalme wa Uingereza yafanyika Scotland
Kwa mara nyingine tena, maandamano makubwa yameshuhudiwa katika mji mkuu wa Scotland, Edinburg kupinga mfumo wa kifalme wa Uingereza.
Waandamanaji hao wanaopinga ufalme wa UK walikusanyika katika Kanisa la Cathedral jijini Edinburg, ambako mwili wa Malkia Elizabeth wa Pili aliyeaga dunia hivi karibuni umelazwa.
Walioshiriki maandamano hayo walikuwa wamebeba mabango na karatasi tupu ambazo hazina maneno yoyote, kuunga mkono 'haki yao ya kuandamana' baada ya watu kadhaa kukamatwa kwa kushiriki maandamano ya aina hiyo.
Baada ya kifo cha Elizabeth II, maandamano ya kupinga ufalme yamefanyika katika nchi nyingi za Jumuiya ya Madola kama vile baadhi ya nchi za Carribean na Pasifiki Kusini, Australia, New Zealand na Canada; na mamlaka ya nchi hizo zinatathmini msimamo wa kumtambua Mfalme Charles III kama kiongozi mkuu wa nchi au kujitenga na Uingereza na kuwa nchi zenye mfumo wa Jamhuri.
Haya yanajiri huku Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern akisema: New Zealand itamweka pembeni mfalme wa Uingereza kama mkuu wa nchi na itakuwa taifa huru.
Wabunge wa Scotland akiwemo Joanna Cherry, wamekosoa kamatakamata hiyo inayofanywa na vyombo vya usalama vya UK, wakisisitiza kuwa, "haki ya kuandamana ina umuhimu mkubwa kwa demokrasia yetu na inapaswa kuruhusiwa."