Umoja wa Ulaya wapendekeza kifurushi cha vikwazo vipya dhidi ya Russia
(last modified Thu, 29 Sep 2022 07:57:46 GMT )
Sep 29, 2022 07:57 UTC
  • Umoja wa Ulaya wapendekeza kifurushi cha vikwazo vipya dhidi ya Russia

Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya jana usiku alipendekeza duru mpya ya vikwazo dhidi ya Moscow; vikiwemo vikwazo katika bei ya mafuta na kuizuia Russia kuuza mafuta yake ya kiasi cha dola bilioni 7.

Mwezi wa nane unapita sasa tangu kuanza vita huko Ukraine vilivyoambatana na taathira zake kubwa za kiisiasa, kijeshi, kiuchumi, kijamii na hata kiutamaduni; huku nchi za Magharibi zikiendelea kuipatia Ukraine silaha na zana mbalimbali za kivita.  

Nchi za Ulaya na Magharibi na hasa Marekani ambazo zinashadidisha vikwazo vyao dhidi ya Shirikisho la Russia na kuipatia Kiev silaha mbalimbali nzito na nyepesi; si tu hazijachukua hatua zozote kuhitimisha vita huko Ukraine bali zimechagiza pakubwa moto wa vita hivyo. 

Shirika la habari la Ufaransa limeripoti kuwa, Ursula von der Leyen Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya amesema kamisheni hiyo ndiyo itakayoainisha msingi wa kisheria wa kupanga bei ya mafuta ya Russia kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa na G-7 ikiwa ni sehemu ya vikwazo vipvya dhidi ya Russia ambavyo vinapasa kusainiwa na nchi 27 za Umoja wa Ulaya. 

Mkuu wa Kamisheni ya Ulaya, Ursula von der Leyen

Von der Leyen ameeleza kuwa Umoja wa Ulaya bado unataka kuizuia Russia kuuza mafuta yake yenye thamani ya dola bilioni 7 na wakati huo huo kuzidisha vizuizi na ukwamishaji kwa bidhaa zinazotoka katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ambazo zinaweza kusaidia katika kampeni ya vita vya Russia.  

Hadi sasa Umoja wa Ulaya umeiwekea Moscow vifurushi saba vya vikwazo vikali tangu Russia ianzishe oparesheni maalumu ya kijeshi dhidi ya Ukraine.

 

Tags