Mkutano wa ushirikiano wa Israel na EU wakosolewa
(last modified Tue, 04 Oct 2022 07:46:54 GMT )
Oct 04, 2022 07:46 UTC
  • Mkutano wa ushirikiano wa Israel na EU wakosolewa

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Palestina yamelaani mkutano wa ushirikiano baina ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Umoja wa Ulaya, wakati huu ambapo utawala huo haramu umeshadidisha hujuma na mbinyo dhidi ya Wapalestina.

Wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu wamekusanyika nje ya jengo la Baraza la Ulaya mjini Brussels, ambako mkutano wa Baraza la Muungano wa EU na Israel unafanyika kwa mara ya kwanza baada ya kupita muongo mmoja.

Watetezi wa haki waliokusanyika mjini Brussels wameshangazwa na kitendo cha kufanyika mkutano huo ghafla baada ya kusitishwa kwa zaidi ya miaka 10. 

Washiriki wa mkutano huo wamekataa kuzungumza na waandishi wa habari, huku wadadisi wa mambo wakisema wamefanya hivyo ili kukwepa kuulizwa masuali mazito juu ya jinai zinazofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina.

Baraza la Muungano  wa EU na Israel limedai kuwa, mkutano huo wa Brussels umejadili vita vya Ukraine, mgogoro wa nishati, na ushirikiano wa pande mbili kwenye nyuga za biashara na mabadiliko ya tabianchi.

Ukatili wa askari Wazayuni dhidi ya Wapalestina

Mkutano huo umepuuza taarifa iliyotolewa na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch muda mfupi kabla ya kuanza kikao chenyewe.

Shirika hilo limesema maafisa wa EU walipaswa kutumia jukwaa la mkutano huo kulaani mfumo wa ubaguzi wa Israel (apartheid), na kutangaza bayana kwamba, kutakuwepo na matokeo mabaya iwapo Israel haitaachana na mwenendo huo.

 

 

Tags