Oct 04, 2022 07:51 UTC
  • Korea Kaskazini yafyatua kombora la balestiki kuelekea Japan

Korea Kaskazini imefyatua kombora lake la balestiki kuelekea upande wa Japan, na kupelekea kusitishwa kwa usafiri wa treni katika baadhi ya maeneo, huku Wajapani katika maeneo ya kaskazini wakitakiwa kujificha.

Majeshi ya Japan na Korea Kusini yamethibitisha kwa nyakati tofauti hatua ya Pyongyang kuvurumisha kombora lake la balestiki la masafa ya kati (IRBM), lililopaa katika anga ya maeneo ya kaskazini mwa Japan.

Mkuu wa Majeshi ya Japan amesema, kombora hilo limefyatuliwa kutoka mkoa wa Jagang wa Korea Kaskazini mapema leo Jumanne, na kwamba hii ni mara ya kwanza kwa Pyongyang kufanya hivyo tokea msimu wa mapukutiko mwaka 2017.

Serikali ya Tokyo imesema kombora hilo la Korea Kaskazini limedondoka katika Bahari ya Pacific, baada ya kupita katika anga ya Japan. Inaarifiwa kuwa, liliruka zaidi ya kilomita 4,500 katika anga ya Japan, na umbali wa kilomita 970 juu ya usawa wa bahari.

Msemaji wa serikali ya Tokyo, Hirokazu Matsuno amesema: Msururu wa vitendo vya Korea Kaskazini yakiwemo majaribio ya makombora yake ya balestiki, unatishia amani na usalama wa Japan, na kwa jamii yote ya kimataifa.

Kiongozi wa Korea Kaskazini akiwapungia mkono askari kabla ya kufyatuliwa kombora

Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida amelaani kitendo hicho, huku Rais wa Korea Kusini, Yoon Suk Yeol akionya kuwa nchi hiyo itatoa jibu mwafaka kwa uchokozi huo wa Pyongyang.

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya Korea Kusini, Japan na Marekani kufanya luteka ya kijeshi ya 'kupambana na nyambizi' katika Peninsula ya Korea.

Tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi hivi sasa, Korea Kaskazini imefanya majaribio zaidi ya 20 ya silaha zake huku sehemu kubwa ya majaribio hayo ikiwa ni kufyatua makombora yake ya balestiki.

Tags