Oct 25, 2022 02:36 UTC
  • Maandamano ya Ulaya dhidi ya kuzorota hali ya kiuchumi

Kufuatia kuenea mgogoro wa kiuchumi katika nchi mbalimbali za Ulaya, wananchi wengi wameandamana katika nchi kama vile Ujerumani, Ufaransa, Uingereza na Romania kulalamikia hali mbaya ya maisha.

Kuongezeka kwa gharama ya maisha, matatizo ya nishati na wasiwasi unaosababishwa na msimu ujao wa baridi kali pamoja na ongezeko la ushuru na ukosefu wa huduma ni kati ya sababu muhimu zaidi za kufanyika maandamano barani Ulaya.

Hali ya uchumi imekuwa mbaya zaidi katika nchi nyingi za Ulaya katika miezi iliyopita na hali hiyo ilitabiriwa huko nyuma. Kwa hakika, sera za uingiliaji za nchi za Ulaya na kufuata kibubusa matakwa ya Marekini katika vita vya Ukraine kumefanya hali kuwa ngumu zaidi kwa nchi za Ulaya.

Nchi hizo ambazo zimejaribu kukabiliana na Russia kwa kutenga bajeti kubwa ya vita ili kuipa Ukraine silaha na zana za kivita, sasa zinakabiliwa na mgogoro wa kiuchumi baada ya zaidi ya miezi minane ya vita hivyo.

Katika upande mwingine, kuwekwa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Russia hasa katika suala la nishati kumesababisha uhamishaji wa gesi kutoka bomba la taifa la Russia kwenda Ulaya kusimama, jambo ambalo limeathiri pakubwa hata uchumi wa Ujerumani ikiwa ni nchi yenye nguvu zaidi barani Ulaya. Hivi sasa Ujerumani inakabiliwa na uhaba mkubwa wa nishati na kwa mujibu wa takwimu za benki kuu ya nchi hiyo, mgogoro wa nishati umeweka uchumi wa Ujerumani kwenye hatari ya kukumbwa na mdororo wa kiuchumi.

Ukosefu wa mafuta na nishati umesababisha kufungwa viwanda vingi vya Ujerumani, na wamiliki wa viwanda vingi vikubwa pia wameonya kuhusu hali mbaya zaidi katika siku zijazo zijazo. Kati ya sekta muhimu zilizoathiriwa zaidi Ujerumani na hali hii ya ukosefu wa nishati ni ile ya utengenezaji wa magari na usafirishaji.

Bomba la Gesi la Nord Stream

Kutokana na kuongezeka kwa tatizo la nishati nchini Ujerumani,  wakuu wa  maduka ya Aldi Nord, wametangaza kwenye Twitter kwamba kuanzia Novemba 2022, matawi yake yote yatafungwa.

Aidha maduka ya bidhaa za kielektroniki ya Saturn na pia maduka ya Galeria kote Ujerumani yametangaza kuwa yanaendelea kukumbwa na matatizo makubwa.

Hali ni hiyo hiyo katika nchi nyingine za Ulaya. Nchini Ufaransa, raia wengi wameingia mitaani kulalaimikia kutolipwa mishahara na ongezeko la gharama ya maisha. Sambamba na maandamano hayo pia kumeitishwa migomo ya nchi nzima na hivyo kupelekea Ufaransa ikumbwe na mgogoro mkubwa. Walimu, makocha, wafanyikazi wa manispaa na madereva wa magari ya umma ni miongoni mwa waliogoma wakidai nyongeza ya mishahara ili kufidia mfumuko wa bei.

Philippe Escande, mchambuzi wa masuala ya uchumi barani Ulaya anasema: Watu wa Ulaya sasa wanakabiliwa na ukosefu mkubwa wa nishati kutokana na ongezeko kubwa la bei ya gesi na umeme hali ambayo imehatarisha sana kuendelea kwa shughuli za makampuni madogo na makubwa. Maendeleo ya kiuchumi hayawezekani bila nishati ya bei nafuu.”

Ulaya kwa sasa inapitia wakati mgumu. Hapo awali, Kansela wa Ujerumani Olaf Schulz, akizungumzia kushadidi migogoro ya kijeshi nchini Ukraine, alisema kuwa nchi za Ulaya zitahisi matokeo ya vita vya Ukraine kwa muda wa miaka mingi ijayo. Aidha ameonya kuhusu madhara ya vita vya Ukraine kwa nishati na usalama wa chakula duniani kote. Hata hivyo, mgogoro wa sasa umeibuka mapema kuliko ilivyotabiriwa.

Nchi za Ulaya pia zilikuwa na matumaini makubwa ya usaidizi na uungwaji mkono wa Marekani, lakini sio tu kwamba zimeachwa peke yao katika mgogoro huo, bali viongozi wa Ulaya sasa wanakiri kwamba Marekani inatumia vibaya hali iliyopo kwa kuziuzia nchi za Ulaya gesi kwa bei ya juu sana.

Maandamano Ujerumani kupinga ughali wa maisha

Hivi sasa nchi nyingi za Ulaya zimekerwa sana na siasa za Washington. Bruno Le Maire, Waziri wa Uchumi na Fedha wa Ufaransa, anasema katika muktadha huu: Mapigano kati ya Russia  na Ukraine na mzozo wa nishati uliosababishwa na mapigano hayo umemalizika kwa faida ya Marekani. Amongeza kuwa Marekani inatumia  vibaya mgogoro uliojitokeza ili kuimarisha  satwa yake katika  uchumi wa dunia.

Fatih Birol, mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati, hivi karibuni alionya kwamba Ulaya itakabiliwa na matatizo makubwa zaidi ya nishati mwaka ujao. Inaonekana kwamba iwapo mgogoro huo utaendelea na msukosuko wa kiuchumi ukazidi, jambo ambalo litapelekea kuendelea kwa maandamano nchini Ujerumani, Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya, si uchumi wa Ulaya pekee bali pia umoja na mshikamano wa Ulaya utasambaratika; suala ambalo likijiri hakuna shaka kwamba litabadilisha jiografia ya kisiasa ya ulimwengu kwa mara nyingine tena.

 

Tags