Kimbunga cha Tropiki cha Nalgae chaua watu 45 nchini Ufilipino
Kwa akali watu 45 wamepoteza maisha baada ya Kimbunga cha Kitropiki cha Nalgae kuipiga Ufilipino.
Hayo yamesemwa leo Jumamosi na Rafaelito Alejandro, Mkurugenzi wa Idara ya Ulinzi wa Raia ya Ufilipino na kuongeza kuwa, watu wengine 33 wamejeruhiwa huku wengine 14 wakitoweka baada ya kujiri kimbunga hicho.
Kimbunga hicho ambacho kinafahamika nchini humo kwa jina la Paeng na ambacho upepo wake unakwenda kwa kasi ya kilomita 95 kwa saa, kilitua katika kisiwa cha Luzon kabla ya jua kuchomoza jana Ijumaa na kusababisha maafa hayo.
Idara ya Hali ya Hewa imeonya kuwa, mvua kubwa zilizosababishwa na kimbunga hicho zitashuhudiwa katika maeneo mengi ya kusini mwa nchi. Imesema huenda Kimbunga cha Nalgae kikaipiga Manila, mji mkuu wa Ufililipino wenye wakazi zaidi ya milioni 13.
Mafuriko makubwa yameripotiwa pia katika maeneo ya katikati mwa nchi, huku shughuli za uokoaji zikiendelea. Kufuatia hali hiyo serikali na wananchi wa Ufilipino wameomba misaada ya dharura hasa ya chakula.
Aprili mwaka huu, watu karibu 60 waliaga dunia kutokana na Kimbunga cha Tropiki cha Megi kilichosababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi katika mkoa wa kati wa Leyte nchini Ufilipino.
Mwaka 2013, kimbunga kikali cha Haiyan kiliua zaidi ya watu elfu 8 huko Uflipino, nchi ambayo inashuhudia vimbunga zaidi ya 20 kila mwaka.