Baraza la Waislamu Marekani lalaani mauaji ya Orlando
https://parstoday.ir/sw/news/world-i9094-baraza_la_waislamu_marekani_lalaani_mauaji_ya_orlando
Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR) limelaani hujuma katika mji wa Orlando nchini Marekani ambapo watu wasiopungua 50 waliuawa jana katika klabu moja huku wengine 53 wakijeruhiwa.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 13, 2016 06:57 UTC
  • Baraza la Waislamu Marekani lalaani mauaji ya Orlando

Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR) limelaani hujuma katika mji wa Orlando nchini Marekani ambapo watu wasiopungua 50 waliuawa jana katika klabu moja huku wengine 53 wakijeruhiwa.

Aliyetekeleza mauaji hayo ametambuliwa na vyombo vya habari vya Marekani kuwa ni Omar Mateen, Mmarekani mwenye asili ya Afghanistan ambaye anadaiwa kuwa muungaji mkono wa kundi la kigaidi la ISIS au Daesh.

Kundi la kigaidi la ISIS limetangaza kuhusika na hujuma hiyo. Katika taarifa, CAIR imetaja mauaji hayo kuwa ni jinai ya chuki ambayo inalaaniwa vikali. Mwenyekiti wa Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani Nihad Awad amesema mauaji hayo yanakiuka misingi ya Marekani na Waislamu. Aidha amesisitiza kuwa ISIS ni kundi haramu lisilowakilisha Waislamu.

Kauli hiyo imekuja punde baada ya mgombea kiti cha urais kwa tiketi ya chama cha Republican Donald Trump kuendeleza matamshi yake ya chuki dhidi ya Uislamu ambapo ametaka hatua kali zaidi zichukuliwe dhidi ya Waislamu Marekani.

Baba yake Omar Mateen amesema mwanae ametekeleza hujuma hiyo kutokana na chuki yake dhidi ya mashoga au kujamiiana watu wenye jinsia moja. Mateen ambaye aliuawa katika hujuma yake hiyo alilenga klabu ambayo ilikuwa mahala pa kukutana mashoga. Makachero wa FBI nchini Marekani wanasema wamewahi kumhoji Mateen mara tatu.