Kuendelea ujasusi wa Israel nchini Uturuki
https://parstoday.ir/sw/news/world-i91736-kuendelea_ujasusi_wa_israel_nchini_uturuki
Maafisa usalama wa Uturuki wamewatia mbaroni watu 44 wengine kwa tuhuma za kulifanyia ujasusi shirika la kijasusi la Israel, MOSSAD nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 15, 2022 22:54 UTC
  • Kuendelea ujasusi wa Israel nchini Uturuki

Maafisa usalama wa Uturuki wamewatia mbaroni watu 44 wengine kwa tuhuma za kulifanyia ujasusi shirika la kijasusi la Israel, MOSSAD nchini humo.

Majasusi hao wa utawala wa Kizayuni wa Israel wametiwa mbaroni nchini Uturuki katika hali ambayo kabla ya hapo Shirika la Kijasusi la Uturuki (MIT) lilikuwa limelionya Shirika la Kijasusi la Israel (MOSSAD) liache mchezo wake wa kufanya ujasusi dhidi ya Wapalestina kwa ajili ya kuwaua kigaidi na kuwasambaratisha ndani ya Uturuki.

Juzi Jumatano, Disemba 14, 2022, duru za habari za Uturuki zilitangaza kuwa, maafisa usalama wa nchi hiyo wameendesha operesheni ya kupambana na ujasusi na kuwatia mbaroni makumi ya majasusi wa Israel waliojificha nyuma ya mgongo wa mashirika yasiyo ya kiserikali NGOs kwa ajili ya kutoa pigo kwa Wapalestina ndani ya Uturuki. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, juhudi za kuwatia mbaroni majasusi wengine 13 kwa tuhuma hizo hizo, zinaendelea.

Kutiwa mbaroni makumi ya majasusi wa Israel huko Uturuki kumefanyika katika hali ambayo serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan, hivi karibunii ilifufua uhusiano wake wa kidiplomasia na utawala wa Kizayuni wa Israel. Licha ya serikali ya Uturuki kujigamba sana kuwa inawaunga mkono wananchi madhlumu wa Palestina, lakini viongozi wa nchi hiyo wanaendelea kung'ang'ania ushirikiano wao na utawala wa Kizayuni ambao mikono yake imejaa damu za wananchi madhlumu wa Palestina kwa zaidi ya miaka 70 sasa. Uhusiano wa Uturuki na Israel unaendelea muda wote katika nyuga tofauti hasa masuala ya usalama na uchumi.

Bendera ya utawala wa Kizayuni wa Israel

 

Hivi karibuni serikali ya Ankara iliwaachilia huru makumi ya majasusi wa Israel ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kufufua uhusiano na utawala ghasibu na katili wa Kizayuni.

Amma na uhakika huu nao inabidi tuujue kwamba, sambamba na juhudi hizo za kufufua uhusiano wa Uturuki na Israel, serikali ya Ankara imewatia mbaroni na kuwafunga jela makumi ya majasusi wa utawala pandikizi wa Kizayuni. Jambo hilo linaonesha ukweli usiopingika kwamba utawala wa kibaguzi wa Israel hauna mwamana hata kidogo. Kadiri unavyojipendekeza kwake hauridhiki na lazima utafanya uafiriti wake. Wachambuzi wa mambo wanasema, hii inaonesha wazi kuwa Israel haitaachana na njama zake kuiweka kwenye wakati mgumu Uturuki na kujaribu kuisambaratisha serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan na kumtoa kwenye ulingo wa siasa za nchi hiyo.

Wachambuzi wa mambo wanasisitiza kuwa, lengo la serikali ya Erdogan la kurejesha uhusiano wa kawaida na baadhi ya nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi pamoja na Misri na utawala wa Kizayuni wa Israel, ni kutaka kujirahisishia njia katika uchaguzi ujao wa Uturuki. Lakini pamoja na hayo, utawala wa Kizayuni umethibitisha kivitendo kuwa, haujali chochote ghairi ya maslahi yake binafsi tu na hauwezi kabisa kuachana na tabia zake za ujasusi wa kiserikali ndani na nje ya ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.

Weledi wa mambo wanasema pia kuwa, kuweko wimbi la vitendo vya kijasusi ndani ya ardhi ya Uturuki ni kengele ya hatari kwa utawala na serikali ya Recep Tayyip Erdogan ya kwamba serikali hiyo haipaswi kuwa na matumaini kabisa ya kupata utulivu kwa kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel. 

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki

 

Kwa upande wake, Sadık Çelik, mtalamu wa masuala ya kisiasa na kimataifa amesema katika mahojiano aliyofanyiwa na Idhaa ya lugha ya Kituruki ya Kitengo cha Matangazo ya Ng'ambo cha IRIB kwamba, ushindi wa wanamapambano wa Palestina dhidi ya utawala wa Kizayuni umethibitisha kuwa, utawala huo ghasibu hauelewi lugha nyingine isipokuwa muqawama na mapambano. Ni mapambano ya silaha tu ndiyo yanayoweza kuilazimisha Israel iheshimu haki za wengine, si mazungumzo.

Kiujumla ni kwamba, kutiwa mbaroni majasusi 44 wa Israel huko Uturuki kunaonesha sehemu ndogo tu ya ujasusi mkubwa unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel nchini humo. Kwa maneno mengine ni kuwa, utawala wa Kizayuni hauwezi kuacha kufanya ujasusi huko Uturuki na katika maeneo yote duniani. Kama tulivyotangulia kusema, kuendelea vitendo hivyo vya kijasusi vya Wazayuni ni kwa hasara ya serikali ya Erdogan; si kwa faida yake na hapa ndipo unapopata maana mtazamo wa wataalamu wa mambo kwamba lengo la Israel ni kuidhoofisha serikali ya Erdogan na chama chake cha Uadilifu na Ustawi na kukitoa kwenye ulingo wa kisiasa nchini Uturuki.