Dunia yaendelea kumuomboleza Pele, akumbukwa kwa wema
Vigogo wa soka na watu mbali mbali duniani wanaendelea kutuma salamu za rambirambi na pole kufuatia kifo cha Pele, mchezaji mashuhuri wa soka wa Brazil ambaye anatajwa kuwa mwanasoka bora zaidi katika historia.
Edson Arantes do Nascimento almaarufu Pele, ameariki dunia akiwa na umri wa miaka 82, familia yake imetangaza Alhamisi. Pele, aliyezaliwa mwaka 1940 amekuwa akiugua saratani ya utumbo kwa muda mrefu. Serikali ya Rais Jair Bolsonaro, anayeondoka madarakani mnamo siku ya Jumapili, imetangaza siku tatu za maombolezo, na kusema katika taarifa kuwa Pele alikuwa mzalendo halisi, akiliinua jina la Brazil kila mahali alipokwenda.
Mrithi wa Bolsonaro, Rais mteule Luiz Inacio Lula da Silva, ameandika kwenye mtandao wa Twitter kuwa, "Wabrazil wachache sana wamefanikiwa kulibeba jina la nchi yetu kama alivyofanya Pele."
Vigogo mbali mbali wa soka duniani wametuma salamu zao za rambirambi. Mshambuliaji wa Paris Saint Germain (PSG) Kylian Mbappe amemuomboleza Pele akisema atakumbukwa milele. “Mfalme wa kandanda hayuko nasi tena lakini mafanikio yake hayatasahaulika. Pumzika kwa amani,” ameandika Mbappe kwenye ukurasa wa akaunti yake ya Twitter.
Naye Fowadi matata wa Ureno Cristiano Ronaldo kupitia Instagram ametuma salama za pole si tu nchini Brazil na hasa kwa familia ya Pele, lakini pia kwa dunia nzima.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni linalotetea nguvu ya michezo duniani kote, UNESCO, limeandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba "limehuzunishwa sana na kifo chake, na kutoa rambirambi kwa watu wa Brazil, na familia pana ya wanakandanda duniani"
Nguli huyo wa soka alitumia muda mwingi alipostaafu kusaidia Umoja wa Mataifa na kazi zake, kama balozi wa mwema wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, na kama bingwa wa UNESCO wa michezo, kutoka mwaka 1994.
Pele pia aliteuliwa kuwa balozi mwema wa mkutano muhimu wa Umoja wa Mataifa wa dunia, huko Rio de Janeiro, mwaka 1992, moja ya mikutano mikuu ya kwanza ya maendeleo ya kimataifa na mazingira inayojikita na mustakabali endelevu zaidi kwa wote.
Katibu mkuu wa mkutano huo, Maurice Strong, amemuelezea Pele kuwa sio tu mwanasoka bora zaidi ulimwenguni, lakini "mtu wa ulimwengu wote", mwenye asili ya Brazil.