Maelfu ya wauguzi wafanya mgomo New York, Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i92712-maelfu_ya_wauguzi_wafanya_mgomo_new_york_marekani
Wauguzi zaidi ya 7,000 katika hospitali mbili kubwa jijini New York nchini Marekani wameanza mgomo baada ya mazungumzo yao na serikali kuhusiana na mazingira yao ya kazi, nyongeza ya mishara na sera za wafanyakazi kugonga mwamba.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 10, 2023 00:14 UTC
  • Maelfu ya wauguzi wafanya mgomo New York, Marekani

Wauguzi zaidi ya 7,000 katika hospitali mbili kubwa jijini New York nchini Marekani wameanza mgomo baada ya mazungumzo yao na serikali kuhusiana na mazingira yao ya kazi, nyongeza ya mishara na sera za wafanyakazi kugonga mwamba.

Chama cha Wauguzi Jimboni New York kimetangaza kuwa, mgomo huo katika hospitali mbili kuu za jiji hilo ulianza jana Jumatatu, baada ya pande mbili hizo kushindwa kufikia makubaliano katika mazungumzo baina yao uliofanyika Jumapili usiku.

Habari zinasema kuwa, wauguzi zaidi ya 3,500 katika Kituo cha Afya cha Montefiore eneo la Bronx na wengine wapatao 3,600 katika Hospitali ya Mount Sinai huko Manhattan waliondoka katika sehemu zao za kazi hiyo jana ili kushiriki mgomo huo.

Muungano huo wa kutetea maslahi ya wauguzi jijini New York unasisitiza kuwa, wahudumu hao wa afya wamelazika kufanya mgomo kudai malipo bora yanayoendana na mfumuko wa bei za bidhaa.

Mgomo na maandamano ya wauguzi New York

Uongozi wa muungano huo umefafanua kuwa, mfumuko mkubwa wa bei na gharama kubwa ya maisha, umepelekea wauguzi katika sekta hiyo na nyingine mbalimbali kudai nyongeza ya mishahara ili kumudu kupanda kwa bei za bidhaa za msingi.

Wauguzi hao wanaogoma walikusanyika jana Jumatatu nje ya hospitali wanakofanya kazi, huku wakipiga nara na kubeba mabango yenye jumbe za kubainisha malalamiko yao; baadhi yakisema 'Hatuwezi kuvumilia tena.'

Wimbi la mfumuko wa bei nchini Marekani lilianza sambamba na kuenea kwa virusi vya corona, lakini vita vya Ukraine vimezidisha makali wa mgogoro huo.