Jan 15, 2023 02:24 UTC
  • Uingereza yahamakishwa na kunyongwa jasusi wake nchini Iran

Waziri Mkuu wa Uingereza ameshindwa kuzuia na kuficha hamaki zake baada ya jasusi wa nchi hiyo kutiwa mbaroni na kunyongwa nchini Iran na amedai kuwa kunyongwa jasusi huyo ni kitendo cha kikatili na cha woga.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Rishi Sunak akitoa matamshi hayo ya kuingilia masuala yasiyomuhusu ya ndani ya Iran kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter na kudai kuwa, eti hatua hiyo haitoachwa hivi hivi bila ya majibu.

Kabla ya hapo pia, James Cleverly, waziri wa mambo ya nje wa Uingereza naye alitoa matamshi ya kuingilia masuala ya ndani ya Iran na kwa mara nyingine alitaka jasusi huyo asinyongwe.

Katika taarifa yake, Cleverly alidai kuwa, serikali ya Iran itambue kwamba tunalifuatilia kwa karibu faili la Alireza Akbari.

Jumatano iliyopita pia, waziri huyo wa mambo ya nje wa Uingereza alidai kuwa, Iran inapaswa kubatilisha hukumu ya kunyongwa Alireza Akbari.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Rishi Sunak

 

Kitengo cha Habari cha Idara ya Mahakama ya Iran, jana Jumamosi kilitangaza kuwa, Alireza Akbari aliyekuwa na uraia pacha wa Iran na Uingereza amenyongwa baada ya kupatikana na hatia ya kufanya ufisadi mkubwa katika ardhi na kuendesha vitendo vya kuhatarisha usalama wa ndani na nje ya Iran kupitia kulifanyia ujasusi shirika la kijasusi la Uingereza MI6. 

Kwa mujibu wa nyaraka na ushahidi uliowasilishwa mahakamani, kwa miaka kadhaa, Akbari alifanya ujasusi kwa maslahi ya serikali ya Uingereza. Alikuwa na uhusiano na shirika la kijasusi la M16 la Uingereza na alifanya mikutano kadhaa na maafisa wa kijasusi wa adui katika nchi mbali mbali. Alihongwa mabilioni ya fedha kufanya ujasusi huo dhidi ya wananchi wa Iran.

Tags