Umoja wa Ulaya washadidisha uingiliaji katika masuala ya ndani ya Iran
(last modified Fri, 20 Jan 2023 02:43:56 GMT )
Jan 20, 2023 02:43 UTC
  • Umoja wa Ulaya washadidisha uingiliaji katika masuala ya ndani ya Iran

Katika muendelezo wa uingiliaji wa Umoja wa Ulaya katika masuala ya ndani ya Iran, Bunge la Ulaya linatafakari na kujadili suala la kuliweka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) katika kile kinachoitwa orodha ya mashirika ya kigaidi.

Katika kikao cha Bunge la Ulaya siku ya Jumanne wiki hii kuhusiana na machafuko ya Iran, wawakilishi wa Bunge hilo walisisitiza ulazima wa kuwekwa IRGC katika orodha ya mashirika ya kigaidi, kushadidisha vikwazo vya 'haki za binadamu' dhidi ya Tehran na kuiwajibisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Abir Al-Sahlani, mjumbe wa Bunge la Ulaya amedai kuwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu linakaribia sana kujumuishwa katika orodha ya mashirika ya kigaidi barani Ulaya. Uingereza pia inatazamiwa kutangaza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kama shirika la 'kigaidi'. Januari 11, Bunge la Uingereza kwa kauli moja liliidhinisha hoja inayoitaka serikali ya nchi hyo kujumuisha IRGC katika orodha ya makundi ya kigaidi. 

Nizamuddin Mousavi, msemaji wa Ofisi ya Spika wa Bunge la Iran, alichapisha ujumbe kwenye ukurasa wake binafsi wa Twitter na kuhutubia Mabunge ya Ulaya, akisema kwamba azimio lolote dhidi ya  Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran litakabiliwa na jibu kali na miswada mkabala kutoka kwa Bunge la Iran. Aidha ameandika kuwa hatua ya nchi za Magharibi ya kuliwekea vikwazo na kulitangaza jeshi la IRGC kuwa ni kundi la kigaidi ni hatua ambayo haina thamani ya kiutendaji bali ni ujanja mbaya tu wa kipuuzi na kipropaganda."
Suala la kuwekwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika orodha ya makundi ya kigaidi liliwasilishwa na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Umoja wa Ulaya mjini Brussels.

Weledi wengi wanaamini kuwa matokeo ya suala hilo yatakuwa wazi mwishoni mwa Februari 2023. Kwa hivyo, haipaswi kutarajiwa kwamba majadiliano juu ya suala hilo yatahitimishwa katika mkutano ujao wa Baraza la Mawaziri wa Mambo ya nje huko Brussels mnamo Januari 23. Inasemekana Ujerumani, Uholanzi na Jamhuri ya Czech ni miongoni mwa nchi zinazounga mkono kuwekwa IRGC katika orodha ya makundi ya kigaidi.
Juhudi zisizo na kifani za Umoja wa Ulaya na taasisi zake, kama vile Bunge la Ulaya, katika uwanja wa kulitangaza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni la kigaidi, kwa hakika ni ishara kuwa nchi za Ulaya zinaifuata Marekani kibubusa bila hata kuhoji hatua zake.

Maafisa wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) wamekuwa mstari wa mbele kuangamiza magaidi wakufurishaji katika eneo

Tarehe 8 Aprili 2019, Rais wa Marekani Donald Trump katika hatua isiyo na kifani katika uga wa kimataifa na kinyume na sheria za kimataifa alitangaza kuwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu  ni shirika la kigeni la 'kigaidi' na kutangaza msururu wa vikwazo dhidi ya jeshi hilo. Kwa hivyo, kwa hatua yake dhidi ya IRGC, utawala wa Trump ulichukua hatua mpya ya kuharibu sheria na kanuni za kimataifa.

Sasa, watawala wa Ulaya, wakati wa urais wa Joe Biden, wanasonga tena kwenye mkondo wa mshikamano wa pande mbili za bahari ya Atlantiki, na wamechukua maamuzu sawa na ya Marekani ya kuzidisha mashinikizo dhidi ya Iran. Kimsingi wakuu wa Ulaya inaonekana wanataka kukariri uzoefu uliofeli wa Marekani katika kuiwekea vikwazo IRGC. Pamoja na hayo kuna nukta kadhaa za kuzingatia kuhusiana na kadhia hii.

Kwanza kabisa, nchi za Umoja wa Ulaya hivi sasa ziko katika hali mbaya na tata ya kiuchumi na kijamii kutokana na kuendelea vita vya Ukraine katika eneo la Ulaya Mashariki na matokeo yake, ambayo yanasababishwa na ushirikiano wao na Marekani katika kuiwekea Russia vikwazo vikubwa, na kuingia katika chokochoko mpya dhidi ya Iran, ambayo kwa hakika itaibua majibu makali kutoka kwa Tehran, na hivyo kuongeza tu matatizo na masaibu ya Ulaya.

Pili, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ni sehemu ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa hakika IRGC ina historia ndefu na athirifu katika kupambana na makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na nchi za Magharibi katika eneo la Asia Magharibi hususan Syria na Iraq. Aidha IRGC  imekuwa na nafasi muhimu katika kuhakikisha utulivu na usalama katika eneo hili. Kwa msingi huo hatua tarajiwa ya  Umoja wa Ulaya ya kutangaza kuwa eti IRGC ni  shirika la 'kigaidi' ni kinyume cha sheria na kanuni za kimataifa na kwa hakika ni hatua inayolenga kudhoofisha amani na usalama wa eneo la Asia Magharibi.
Suala jengine ni matokeo yanayoweza kusababishwa na hatua za taasisi za Umoja wa Ulaya likiwemo Bunge la Ulaya na Kamisheni ya Umoja wa Ulaya za kulitangaza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kuwa ni shirika la 'kigaidi', jambo ambalo kwa hakika litakabiliwa na jibu madhubuti kutoka kwa Tehran.

Brigedia Jenerali Rasoul Sanaei-Rad, mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya IRGC amesema: Kuitangaza IRGC kuwa ni shirika la kigaidi kutaongeza kiwango cha mvutano na Uingereza, washirika wake wa Ulaya na Marekani. Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni sehemu ya jeshi rasmi na la kisheria la nchi, na hatua yoyote dhidi yake inachukuliwa kuwa ni hatua dhidi ya mfumo na mamlaka ya kujitawala ya Iran, na bila shaka hatua kama hiyo haitapita bila kujibiwa.

Tags