Watu 10 wauawa kwa kupigwa risasi kwa umati California, Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i93194-watu_10_wauawa_kwa_kupigwa_risasi_kwa_umati_california_marekani
Zaidi ya watu kumi wameuawa kwa kupigwa risasi kwa umati huko Monterey Park, California nchini Marekani wakati sherehe za Mwaka Mpya wa Kichina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 23, 2023 01:29 UTC
  • Watu 10 wauawa kwa kupigwa risasi kwa umati California, Marekani

Zaidi ya watu kumi wameuawa kwa kupigwa risasi kwa umati huko Monterey Park, California nchini Marekani wakati sherehe za Mwaka Mpya wa Kichina.

Ufyatuaji risasi huo ulifanyika Jumamosi usiku katika eneo la Monterey Park, mashariki mwa Los Angeles katika jimbo la California, karibu na eneo la sherehe ya Mwaka Mpya wa Kichina.

Kulingana na ripoti, takriban watu 16 wamepigwa risasi, wakiwemo kumi ambao waliaga dunia kutokana na majeraha ya risasi.

Mashuhuda wawili walisema walisikia milio ya risasi lakini awali walidhani ilikuwa fataki za kuadhimisha Mwaka Mpya wa Lunar.

Makumi ya maelfu ya watu walikuwa wamehudhuria tamasha hilo mapema tamasha la siku mbili la Mwaka Mpya wa Kichina. Sherehe za Mwaka Mpya wa Kichina zimeanza rasmi Januari 22, 2023, na zinatazamiwa kumalizika tarehe 1 Februari.

Tukio hilo ni la hivi punde zaidi ni katika mfululizo wa mashambulizi yanayolenga Wamarekani wenye asili ya  Asia, Visiwa vya Pasifiki (AAPI) kote Marekani.

Uhalifu dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Asia haswa China uliongezeka katika miaka ya hivi karibuni, haswa wakati wa janga la corona huku wataalam wakisema hali hii kwa sehemu kubwa imechagiwa na matamshi ya kibaguzi kutoka kwa rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, ambaye mara kwa mara alitumia maneno ya ubaguzi wa rangi dhidi ya Wachina. Trump mara kwa mara aliitaja corona kama "Virusi vya Uchina".

Kati ya Machi 2020 na Machi 2022, zaidi ya matukio 11,400 ya chuki dhidi ya Waamerika wa Asia yaliripotiwa kote Marekani, kulingana na ripoti ya Stop AAPI Hate, muungano wa kitaifa unaofuatilia matukio kama hayo na watetezi wa kupambana na uhalifu wa chuki dhidi ya Waamerika wenye Asia na Pasifiki.

Ufyatulianaji wa risasi kiholela ni jambo lingine la wasiwasi ambapo mwaka uliopita Marekani ilikumbwa na visa zaidi ya 600 vya ufyatulianaji risasi mwaka 2022, karibu mara mbili ya idadi iliyorekodiwa miaka minne iliyopita wakati kulikuwa na visa 336.

Kiwango cha vifo vinavyosababishwa na silaha za moto kinazidi kuongezeka nchini Marekani. Aidha ununuzi wa bunduki ulipanda hadi viwango vya rekodi mnamo 2021 na 2022.