EU yaendeleza msimamo wa uhasama dhidi ya Iran
(last modified Tue, 24 Jan 2023 02:45:18 GMT )
Jan 24, 2023 02:45 UTC
  • EU yaendeleza msimamo wa uhasama dhidi ya Iran

Umoja wa Ulaya umeendeleza misimamo yake ya uhasama kwa Iran kwa kuiwekea vikwazo vipya.

Sweden ambayo ni mwenyekiti wa sasa wa kiduru wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana Jumatatu iliendeleza misimamo ya uingiliaji wa nchi za Magharibi katika masuala ya ndani ya Iran kwa kutangaza kuwa: Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa katika kikao chao cha jana walipanga kupasisha kifurushi kipya cha vikwazo dhidi ya Iran kwa kisingizio cha masuala ya haki za binadamu na kwa madai kwamba Iran inashirikiana na Russia katika vita dhidi ya Ukraine.  

Uingereza pia jana Jumatatu iliwaweka shakhsia 5 na taasisi mbili za Kiirani katika ordha yake ya vikwazo dhidi ya Iran ikiwa ni katika muendelezo wa misimamo ya uhasama ya serikali ya London dhidi ya Tehran. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliwahi kutahadharisha kuhusu hatua za uingiliaji za nchi za Magharibi katika masuala yake ya ndani na kueleza kuwa vitendo hivyo havitaachwa bila ya jibu.   

Akizungumza wiki hii katika mkutano na waandishi wa habari hapa Tehran, Nasser Kan'ani Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alizitaja hatua hizo za Wamagharibi dhidi ya Iran kuwa zisizokubalika, zisizojenga na zinazopingana na sheria za Umoja wa Mataifa na matamko ya kimataifa. Amesema nchi hizo hazina haki ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine huru duniani. 

Nasser Kan'ani ameashiria namna Iran ilivyo na haki ya kujibu na kuonyesha radiamali yake kwa vikwazo dhidi yake na kuongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itajibu kwa wakati hatua zozote haribifu dhidi yake kwa kustafidi na suhula na uwezo na haki yake ya kisheria ili kuzuia mienendo ghalati na isiyo na manufaa ya Wamagharibi.  

Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza pia kuwa, hatua zozote za kuingilia masuala ya ndani ya Jamhuri ya Kiislamu hazitaachwa bila ya jibu na Iran haitaathiriwa na mashinikizo ya kisiasa ambayo yanatekelezwa katika baadhi ya nyanja ili kufikia mapatano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.  

 

Tags