Jan 25, 2023 11:48 UTC
  • Nchi za Kiislamu zalaani kuvunjiwa heshima tena Qurani Uholanzi

Mataifa na jumuiya za Kiislamu kote duniani zimelaani kitendo cha kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu nchini Uholanzi, siku chache baada ya kutokea uafriti mwingine wa kukichoma Kitabu hicho Kitakatifu cha Waislamu nchini Sweden.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Lebanon, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu, Qatar, Misri, Jordan, na Palestina ni miongoni mwa nchi zilizochukua msimamo dhidi ya kitendo hicho cha kuchukiza nchini Uholanzi.

Wakati huo huo, Nayef Al-Hajraf, Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi, na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC wametoa taarifa za kulaani wimbi hilo la kuvunjwa heshima Qurani Tukufu katika nchi za Ulaya.

Juzi Jumatatu, Edwin Wagensveld, mwanasiasa wa mrengo wa kulia na mwenye chuki kubwa dhidi ya Uislamu wa Uholanzi, kwa kejeli dharau na majivuno alichana kurasa za Qurani Tukufu katika mji wa Hague kadamnasi ya watu na kamera.

Mwanasiasa huyo alienda mbali zaidi na kuzitia moto kurasa hizo za Qurani Tukufu alizozichana, kitendo ambacho kimewaghadhabisha na kuumiza nyoyo na hisia za Waislamu kote duniani.

Jumamosi iliyopita, kiongozi mwingine wa chama cha mrengo wa kulia na mwenye chuki dhidi ya Uislamu wa Denmark, Rasmus Paludan, alichoma moto nakala ya Kitabu Kitakatifu cha Mwenyezi Mungu nje ya ubalozi wa Uturuki katika mji mkuu Sweden.

Sheikh Isa Qassim

Huku hayo yakijiri,  Sheikh Isa Qassim, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Bahrain amelaani kitendo hicho cha kuvunjiwa heshima Qurani Tukufu huko Stockholm, mji mkuu wa Sweden na kueleza kuwa, jinai hizo za chuki hazipaswi kutazamwa kwa jicho la uhuru wa maoni na kujieleza.

Kiongozi huyo mashuhuri wa kidini nchini Bahrain amebainisha kuwa, jinai hizo hazifai kuonekana tu kama jinai za mtu binafsi, bali zinapaswa kutazamwa kama jinai za kiserikali.  

Tags