Iran, dunia zalaani shambulio la kigaidi lililoua 88 msikitini Pakistan
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani shambulio la kigaidi lililotokea jana msikitini kaskazini magharibi mwa Pakistan na kuua na kujeruhi makumi ya watu.
Nasser Kan'ani amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalaani kitendo chochote cha kigaidi ambacho kinahatarisha usalama na uthabiti wa nchi na wananchi wa Pakistan.
Amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa mkono wa pole kwa serikali, kwa wananchi wa Pakistan na familia za wahanga wa shambulio hilo. Vile vile amewaombea dua na msamaha wa Mwenyezi Mungu wote waliouawa kwenye shambulio hilo la kigaidi kama ambavyo amewaombea pia afueni ya haraka majeruhi.
Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umetoa taarifa na kulaani mlipuko huo wa kigaidi uliotekelezwa katika Msikiti wa Waislamu wa Kishia huko Pakistan. Stephane Dujaric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema umoja huo unalaani vikali hujuma hiyo ya kigaidi.
Dujaric amesema Antonio Guterres amebainisha wasiwasi wake kuhusu mashambulizi yanayotekelezwa kuwalenga raia huko Pakistan, na ametaka kusitishwa hujuma hizo.
Huku hayo yakijiri, Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imelaani pia shambulio hilo lililopelekea kuuawa makumi ya Waislamu wakitekeleza ibada msikitini nchini Pakistan. Taarifa ya harakati hiyo ya muqawama imeeleza kuwa, "Kushupalia makundi ya kitakfiri kutenda jinai za kutisha dhidi ya usalama na uthabiti wa nchi za Kiislamu kunahitaji jibu la ushirikiano wa nchi za Waislamu, ambazo zinapasa kukabiliana na wauaji wanaovaa vazi la dini."
Haya yanajiri huku idadi ya watu waliuawa shahidi katika shambulizi hilo la kujilipua kwa bomu lililotokea katika msikiti wa mji wa Peshawar huko kaskazini magharibi mwa Pakistan ikikaribia 90. Maafisa wa hospitali za mji huo wanasema idadi ya waliofariki dunia imefikia 88, na huenda ikaongezeka kutokana na idadi kubwa ya majeruhi wa hujuma hiyo.