WHO: COVID-19 bado ni dharura ya afya ya umma duniani
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema, ugonjwa wa COVID-19 bado ni tishio la afya ya umma duniani na kwa mantiki hiyo dharura itokanayo na janga hilo iliyotangazwa miaka mitatu iliyopita itaendelea.
Kauli ya Dkt, Tedros iliyomo kwenye taarifa aliyotoa jana Jumatatu mjini Geneva inafuatia ushauri aliopatiwa na kikao cha 14 cha Kamati ya kimataifa ya WHO kuhusu dharura za magonjwa kilichokutana Ijumaa kutathmini iwapo bado COVID-19 ni dharura ya afya ya umma au la, wakati jana mripuko huo wa COVID-19 uliingia mwaka wa nne.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO amesema “nakubaliana na ushauri uliotolewa na kamati kuhusu janga la COVID-19 linaloendelea na kubaini ya kwamba janga hilo linaendelea kuwa tishio la dharura ya afya ya umma inayotia hofu duniani, PHEIC. Nakubali maoni ya Kamati kuwa janga la COVID-19 pengine liko kweye kipindi cha mpito na nashukuru ushauri wa kamati kwamba tupite kipindi hiki cha mpito kwa umakini na kuhimili madhara yake.”

Kamati hiyo ya kimataifa ya WHO imekubaliana kuwa COVID-19 inasalia kuwa ugonjwa hatari wa kuambukiza wenye uwezo wa kuharibu afya na mifumo ya afya na kwamba kufikia kiwango cha kinga dunia nzima iwe kwa kudhibiti maambukizi au kwa chanjo kunaweza kudhibiti madhara na vifo vitokanavyo na COVID-19 lakini kuna shaka kidogo ya kwamba virusi hivyo vitasalia moja kwa moja kwenye miili ya binadamu na wanyama katika siku za usoni. Ni kwa msingi huo, Kamati hiyo imesema hatua za muda mrefu kwenye afya ya umma zinahitajika.
Wiki iliyopita WHO ilitangaza kuwa bado COVID-19 inaendelea kusababisha vifo ambapo China inaongoza kwa kuwa na vifo vingi zaidi tangu mwisho wa mwezi uliopita wa Desemba.../