Malaysia: Chuki dhidi ya Uislamu inapaswa kujinaishwa
Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Malaysia ametoa mwito wa kujinaishwa chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Abdul Razak Ahmad, mjumbe maalumu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Malaysia alitoa mwito huo jana Ijumaa na kusisitiza kuwa, kuna haja kwa ulimwengu wa Kiislamu kutoa jibu zito kwa vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi za Magharibi.
Sanjari na kulaani kitendo cha kuchomwa moto nakala ya Qur'ani mbele ya ubalozi wa Russia nchini Denmark, nje ya ubalozi wa Uturuki nchini Sweden na pia huko Uholanzi, Ahmad amesema chuki dhidi ya Uislamu inapaswa kutambuliwa kama kosa la jinai hususan katika nchi za Waislamu.
Mjumbe huyo maalumu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Malaysia amebainisha kuwa, wasiwasi mkubwa uliopo hivi sasa ni juu ya njama za kutaka kueneza kote duniani chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Ameongeza kuwa, majungu hayo ya kueneza chuki dhidi ya Uislamu katika pembe zote dunia yanapikwa na Wamagharibi katika hali ambayo, tasiwra ya Uislamu imeendelea kupotoshwa, huku 'wanaolishwa' propaganda za kuuchukia Uislamu wakiwa hawana ufahamu mkubwa kuihusu dini hiyo tukufu.
Kuvunjiwa heshima Qur’ani Tukufu kumezusha wimbi la hasira na malalamiko makali ya Waislamu kote duniani, na watetezi wa uhuru wa itikadi pia wamelaani vikali kuchomwa moto nakala ya kitabu hicho kitakatifu.
Abdul Razak Ahmad, mjumbe maalumu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Malaysia amesema Wamagharibi wanapaswa kutazama mambo kwa uhalisia na kusisitiza kuwa, uhuru wa kujieleza na uhuru wa maoni kamwe hauwezi kutumiwa kuhalalisha vitendo vya kudhalilisha dini nyinginezo.