Kufukuzwa "Ilhan Omar", mbunge Mwislamu, katika Kamati ya Kongresi ya Marekani
Ilhan Omar, mwakilishi mwanamke wa Kiislamu wa chama cha Democratic amefukuzwa katika Kamati ya Mahusiano ya Kigeni ya Baraza la Wawakilishi la Marekani kwa kuukosoa utawala wa Kizayuni wa Israel. Baraza la Wawakilishi la Marekani lilimfukuza Omar kutoka Kamati ya Mahusiano ya Kigeni kwa kura 218 zilizounga mkono za Warepublican na kura 211 zilizopinga za Wademokrati.
Ilhan Omar amekuwa akikabiliwa na mashinikizo kwa muda mrefu kutokana na matamshi yake ya kukosoa siasa za Israel na kulaani jinai na uhalifu unaofanywa na utawala huo ghasibu dhidi ya watu wa Palestina. Omar ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati ya Mahusiano ya Kigeni ya Baraza la Wawakilishi daima amekuwa na misimamo maalumu dhidi ya siasa za utawala wa Kizayuni wa Isael. Mara kwa mara amekuwa akikosoa hatua za Tel Aviv dhidi ya Wapalestina hususan mashambulizi ya kikatili ya utawala huo dhidi ya raia wasio na hatia na kuitaka Washington itazame upya suala la kutoa misaada ya kifedha na kijeshi kwa Israel. Kwa sababu hiyo, yeye na Rashida Tlaib, mwakilishi mwingine Mwislamu wa Baraza la Wawakilishi la Marekani, wamekuwa chini ya mashinikizo kwa muda mrefu kutokana na misimamo yao dhidi ya Israel na upinzani dhidi ya sera za Marekani za kuiunga mkono Tel Aviv.

Siku chache zilizopita pia Ilhan Omar alitangaza kuwa, serikali ya Israel inamfutilia mbali na kumuua yeyote anayekosoa uvamizi wa maeneo ya Palestina.
Misimamo ya Ilhan Omar na Rashida Tlaib daima imekuwa kinyume na siasa za Marekani na wamekuwa wakilaani jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina. Wawakilishi hawa wawili wa Kongresi ya Marekani daima wamekuwa wakipinga himaya na uungaji mkono wa Marekani kwa sera na uhalifu wa Israel, kwa sababu hiyo wamekuwa wakishinikizwa na lobi amilifu za Israel huko Marekani kwa visingizio mbalimbali vya kisiasa. Kwa mfano tu hivi karibuni walizuiwa kufanya safari katika ardhi zinaokaliwa kwa mabavu za Palestina. Wabunge hawa wawili pia wanaunga mkono kampeni ya kimataifa ya kuisusia Israel maarufu kama The Boycott, Divestment, Sanctions (BDS).

Msimamo wa wawakilishi hawa wawili wa Kongres wa kupinga sera za Israel, unashuhudiwa huku wakiwa chini ya shinikizo kwa sababu wao ni Waislamu, na wawakilishi wengi wa Bunge la Marekani hususan wa chama kinachodhibiti bunge cha Republican, hawastahamili uwepo wao katika Kongresi katika kalibu ya sera za kupiga vita Uislamu (Islamophobia); kwa kadiri kwamba sasa Warepublican wameanza kampeni ya kuwafukuza kabisa katika Kongresi ya Marekani. Katika mkondo huo Mike Waltz, mwakilishi wa Republican wa Baraza la Wawakilishi, anasema: “Israel na Marekani zina maadili ya pamoja na wale wanaounga mkono maadili haya ndio wanaostahili kuwa katika Kamati ya Mahusiano ya Kigeni; chuki dhidi ya Wayahudi haina nafasi katika kamati hii.”
Ilhan Omar amekosoa uamuzi wa Kevin McCarthy, Spika wa Bunge la Marekani, wa kumuondoa katika Kamati ya Mahusiano ya Kigeni na kuutaja uamuzi huo kuwa wa kibaguzi na katika muktadha wa chuki dhidi ya wageni.
Licha ya mashinikizo hayo yote, harakati za Waislamu katika medani za kisiasa za Marekani zimeongezeka kiasi kwamba kwa mujibu wa uchambuzi wa Baraza la Mahusiano ya Kiislamu ya Marekani CAIR kwa kifupi, linalotetea haki za kiraia, na vilevile uchambuzi wa Jetpack, shirika lisilo la kibiashara linalolenga kuongeza uwakilishi wa Waislamu katika siasa za Marekani, hadi sasa Waislamu wameshinda viti visivyopungua 83 katika chaguzi za katikati ya muhula za serikali za mitaa, majimbo na shirikisho.

Inaonekana kuwa Israel inafanya jitihada kubwa za kuendeleza ushawishi wake nchini Marekani, kwa kadiri kwamba sauti yoyote ya upinzani dhidi ya Israel inatambuliwa kuwa mstari mwekundu kwa serikali za Marekani.
Hata hivyo, licha ya kufukuzwa Ilhan Omar katika Kamati ya Masuala ya Kigeni na juhudi za kueneza chuki dhidi ya Uislamu na kuzidishwa ushawishi wa lobi za Israeli huko Marekani, lakini inaonekana kuwa sera za kupinga uhalifu na jinai za Israeli zinaongezeka siku baada ya nyingine kati ya jamii ya nchi hiyo.