Russia: Tutatumia silaha zozote iwapo Ukraine itaishambulia Crimea
https://parstoday.ir/sw/news/world-i93698-russia_tutatumia_silaha_zozote_iwapo_ukraine_itaishambulia_crimea
Russia imetoa onyo kali na kusisitiza kuwa, shambulio lolote la Ukraine dhidi ya eneo la Crimea litaiepelekea Moscow kutumia 'silaha za aina yoyote' kujibu mapigo na kujilinda.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 05, 2023 06:54 UTC
  • Russia: Tutatumia silaha zozote iwapo Ukraine itaishambulia Crimea

Russia imetoa onyo kali na kusisitiza kuwa, shambulio lolote la Ukraine dhidi ya eneo la Crimea litaiepelekea Moscow kutumia 'silaha za aina yoyote' kujibu mapigo na kujilinda.

Indhari hiyo imetolewa na Dmitry Medvedev, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia katika ujumbe wake aliotuma kwenye mtandao wa Twitter na kuongeza kuwa: Shambulio dhidi ya Crimea ni shambulio dhidi ya Russia, na hatua hiyo itachochea zaidi mgogoro.

Rais huyo wa zamani wa Russia amebainisha kuwa, 'waraibu a mihadarati wa Ukraine' wanapaswa kufahamu kuwa, hujuma yoyote dhidi ya Crimea itakabiliwa na jibu lisiloepukika kwa kutumia silaha za aina yoyote na mbinu zozote.

Medvedev amesema iwapo Crimea itashambuliwa, hakuna mazungumzo yoyote yatafanyika juu ya shambulio hilo, na kitakachojiri, ni wimbi la mashambulizi ya ulipizaji kisasi ambayo yataiteketeza Ukraine.

Onyo la Russia limekuja baada ya Igor Klymenko, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ukraine kusema kuwa, Kiev imeunda brigedi maalumu za jeshi, gadi ya mipaka, na askari polisi kwa ajili ya kufanya operesheni za kuikomboa Crimea na Donbass.

Kombora la hypersonic la Russia

Mwishoni mwa mwezi uliopita pia, Nedy Price Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani alidai kuwa kisiwa cha Crimea ni sehemu ya ardhi ya Ukraine, na kwamba Washington itaipatia serikali ya Kiev zana na silaha inazohitaji kwa ajili ya kukomboa ardhi yake.

Hii ni katika hali ambayo, kisiwa cha Crimea kilijiunga na Russia mwaka 2014 baada ya kufanyika kura ya maoni ambapo zaidi ya asilimia 96 ya washiriki katika kura hiyo waliunga mkono suala hilo.