Nebenzya: Nchi za Magharibi zimeazimia kikwelikweli kuiangamiza Russia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i94228-nebenzya_nchi_za_magharibi_zimeazimia_kikwelikweli_kuiangamiza_russia
Vasily Alekseyevich Nebenzya, Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, nchi za Magharibi zimeazimia kikwelikweli kuiangamiza nchi yake, hivyo Moscow haina chaguo jingine isipokuwa kujihami kwa ajili ya kulinda utambulisho na mustakbali wake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 19, 2023 08:20 UTC
  • Nebenzya: Nchi za Magharibi zimeazimia kikwelikweli kuiangamiza Russia

Vasily Alekseyevich Nebenzya, Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, nchi za Magharibi zimeazimia kikwelikweli kuiangamiza nchi yake, hivyo Moscow haina chaguo jingine isipokuwa kujihami kwa ajili ya kulinda utambulisho na mustakbali wake.

Nebenzya amesema hayo na kuzishutumu nchi za Magharibi kwa kufanya njama za kuiangamiza kikamilifu Russia akisisitiza kuwa, Wamagharibi hawapendi kabisa kuona kuna mfumo wa kiusalama wa Ulaya ambao pembeni yake ipo pia Russia.

Balozi huyo wa Russia katika Umoja wa Mataifa pia amezishutumu nchi za Magharibi kwa kukwamisha utekelezaji wa makubaliano ya amani.

Ikumbukwe kuwa tarehe 12 Februari 2015, na baada ya mazungumzo ya kidiplomasia baina ya viongozi wa Ufaransa na Ujerumani, kulitiwa saini makulibano ya kutoshambuliana baina ya viongozi wa Ukraine na watu wanaopigania kujitenga. Makubaliano hayo ambayo sherehe za kutiwa kwake saini zilihudhuriwa pia na Rais wa Russia, yalianza kutekelezwa tarehe 15 Februari 2015 na yanajulikana kwa jina la Makubaliano ya Minsk. Pamoja na hayo lakini, jeshi la Ukraine likiungwa mkono na madola ya Magharibi, limekuwa likivunja mara kwa mara makubaliano hayo.

Vita vya Ukraine vinaangamiza kila kitu

 

Nchi za Magharibi zinaendelea kuisheheneza silaha Ukraine katika hali ambayo hata matokeo ya karibuni kabisa ya maoni yanaonesha kuwa, sehemu kubwa ya wananchi wa Ujerumani wanapinga siasa za nchi yao za kuchochea mapigano huko Ukraine; wanapinga mpango wa nchi yao wa kuipa Kyiv vifaru na wanaamini kwamba siasa hizo zinazidi tu kuchochea moto wa vita na mapigano ya muda mrefu huko mashariki mwa Ulaya.

Russia nayo imekuwa ikizishutumu na kuzilaumu mara kwa mara nchi za Magharibi kwa kutoheshimu makubaliano ya kusimamisha vita na inasisitiza kuwa, wanaoathirika zaidi na uchochezi huo wa Magharibi ni wananchi wa Ukraine.