Wallace: Vikwazo vya EU dhidi ya Russia vinahudumia maslahi ya Marekani
(last modified Sat, 25 Feb 2023 02:42:43 GMT )
Feb 25, 2023 02:42 UTC
  • Wallace: Vikwazo vya EU dhidi ya Russia vinahudumia maslahi ya Marekani

Mbunge wa Bunge la Ulaya amevitaja vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Russia kuwa huduma kwa maslahi ya Marekani na uwendawazimu usio na kifani kwa niaba ya watu wa Ulaya.

Mick Wallace, Mbunge wa Ireland katika Bunge la Ulaya amesema hayo na kuongeza kuwa, EU imejidhalilisha na kujitweza kwenye mgogoro wa Ukraine, kwa kufuata kibubusa amri na sera za Marekani kwa madhara ya watu wa Ulaya.

Wallace amesema Wamarekani hawakutaka Ulaya inunue gesi ya bei nafuu kutoka Russia, ili kwa utaratibu huo Washington iweze kuziuzia nchi za Ulaya gesi yao 'chafu' na kwa bei ya juu, mara nne zaidi ya Russia.

Mbunge huyo wa Bunge la Ulaya raia wa Ireland ameeleza bayana kuwa, biashara katika nchi za Ulaya hivi sasa zinapitia kipindi kigumu, na kwamba vikwazo vya EU dhidi ya Russia havijawa na maslahi yoyote kwa nchi za Ulaya.

Mick Wallace, Mbunge wa Ireland katika Bunge la Ulaya

Wallace amezitaka nchi za Ulaya kufanya maamuzi ambayo yana maslahi kwao juu ya nishati na gesi ya Russia. Amesisitiza kuwa, "Umekuwa mwaka mmoja wa fedheha kwa Umoja wa Ulaya. Tunachukua maamuzi ambayo ni mazuri kwa Marekani na NATO, lakini hayana umuhimu wowote kwa watu wa Ulaya."

Mwanasiasa huyo wa Ireland amesema vikwazo hivyo vya EU dhidi ya Russia katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita vimekuwa na taathira hasi zaidi kwa nchi za Ulaya badala ya Moscow.

Tags