China yaikosoa vikali Marekani
Rais Xi Jinping wa Uchina, amehutubu kwenye mkutano wa mwaka wa chama tawala cha Kikomunisti, ambapo ameishambulia vikali Marekani na kusema: Washington inaongoza kampeni ya "kuzuia, kuzingira na kuikandamiza" China.
Rais Xi Jinping ambaye hivi karibuni ataanza kuhudumu katika muhula wake wa tatu kama rais, amengeza kuwa: Beijing inakabiliwa na changamoto kubwa zisizo na kifani kutoka nchi za Magharibi."
Aidha amesema katika miaka mitano iliyopita, nchi za Magharibi zimeibua matatizo na kuiwekea China vikwazo ili kupunguza ukuaji wa uchumi wake.
Sera za Marekani dhidi ya China zimeongezeka katika nyanja mbalimbali tangu urais wa Donald Trump. Bila shaka, tokea zama za urais wa Barack Obama, sera za Marekani zimekuwa zikilenga katika kuizingira China na kudhoofisha nguvu zake. Kwa kutuma vikosi vyake katika eneo la Mashariki ya Asia, hasa katika eneo la maji ya bahari, Marekani kimsingi imeizingira China kijeshi. Pamoja na hayo amesema vita vya kibiashara vya Marekani dhidi ya China vilianza wakati wa utawala wa Donald Trump ambaye aliiwekea nchi hivyo vikwazo kadhaa vya kibiashara.
Mohsen Ruy Sefat, mtaalamu wa masuala ya kisiasa, anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: "Kuna mitazamo miwili nchini Marekani kuhusu China. Mtazamo wa kwanza unaichukulia China kama nchi ambayo, ikiwa haitadhibitiwa, itahatarisha kwa kiasi kikubwa ubeberu wa kimataifa wa Marekani. Walio na mtazamo huo wanasisitiza kuhusu kudhibitiwa China. Mtazamo wa pili unasisitiza ushirikiano wa kimkakati na China kama mshindani. Hata hivyo, inaonekana kwamba mtazamo wa kwanza ndio unaotekelezwa na Marekani dhidi ya China."

Kwa msingi huo, Rais wa China katika kikao cha wajumbe wa Chama cha Kikomunisti amesisitiza kwamba nchi hiyo lazima iwe na ujasiri wa kupigana kwa sababu inakabiliwa na mabadiliko ya kimsingi katika mazingira ya ndani na kimataifa. Hii ina maana kwamba kwa mtazamo wa China, Marekani inavuka mstari mwekundu wa Beijing, hasa kuhusiana na suala la Taiwan. Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nje wa China pia aliionya Marekani kuhusu hilo.
Marekani inatumia njia tatu kukabiliana na China ambazo ni kadhia ya Taiwan, haki za binadamu na vikwazo vya kibiashara. Katika maudhui hizo tatu kadhia ya Taiwan ina umuhimu zaidi kwa China.
Bahram Jahed, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema kuhusiana na hilo: "Moja ya malengo ya Marekani ya kutumia mashinikizo maradufu dhidi ya China ni kuilazimisha kuingia katika medani ya mashindano ya silaha ili kuifanya itumbukie katika hatima ya Umoja wa Kisovieti ambao hatimaye ulisambaratika. China imeonyesha kwa vitendo kwamba inatumia busara na haiwezi kutumbukia katika mtego huo wa Marekani."
Kwa vyovyote vile, kauli ya Xi Jinping kwenye Bunge la Chama cha Kikomunisti kwamba China ijitegemee yenyewe kwa kuwa taifa kubwa la watu bilioni 1.4 ni suala muhimu linaloashiria kuendelea kwa sera ya China ya kujitegemea ili kuweza kukabiliana na uhasama wa Marekani, hasa katika sekta ya uchumi na teknolojia. Nukta muhimu aliyosisitiza Rais Xi Jinping ni hii kwamba, China haiwezi kutegemea masoko ya kimataifa kujitetea na kujinusuru katika makabiliano yake na Marekani.