WHO: Nchi nyingi hazina sera za kudhibiti matumizi makubwa ya chumvi
(last modified Fri, 10 Mar 2023 07:05:17 GMT )
Mar 10, 2023 07:05 UTC
  • WHO: Nchi nyingi hazina sera za kudhibiti matumizi makubwa ya chumvi

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya kuwa, karibu robo tatu ya nchi wanachama wa taasisi hiyo hazina sera za kupunguza kwa lazima matumizi ya juu ya chumvi.

Ripoti mpya ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa imeonya kuwa, aghalabu ya nchi duniani zimebakia nyuma katika kufanikisha jitihada za pamoja za kupunguza matumizi ya chumvi kwa asilimia 30 kufikia mwaka 2025. 

WHO imesema ni nchi tisa tu kati ya 194 wanachama wake zenye sera madhubuti za kudhibiti matumizi ya kupindukia ya chumvi. Ripoti ya Shirika la Afya Duniani imesema nchi hizo ni Brazil, Chile, Jamhuri ya Czech, Lithuania, Malaysia, Mexico, Saudi Arabia, Uhispania na Uruguay.

Wataalamu wa afya wanasisitiza kuwa, kuna haja kwa serikali na mamlaka husika duniani kuchukua hatua za kivitendo na za uhakika kuhakikisha kuwa matumizi ya kupindukia ya chumvi kwa mwanadamu yanapunguzwa.

Katika hali ambayo chumvi inaongeza ladha katika milo na pia ni kiungo kinachohitajika mwilini ili mifumo ya mwili iweze kufanya kazi vizuri, lakini wataalamu wa afya wametahadharisha kuhusu hatari na madhara ya kiafya ya utumiaji wa kupindukia wa bidhaa hiyo.

Tom Frieden, Rais na Afisa Mkuu wa Mtendaji wa taasisi ya Resolve to Save Lives amesema, ripoti hiyo ya WHO inaonesha wazi kwamba, kuna haja kwa serikali za dunia kuzinduka na kubuni sera za kupunguza kwa lazima matumizi ya juu ya chumvi, na kuhakikisha kuwa zinatekelezwa, ili kupunguza vifo vya mshtuko wa moyo na kiharusi.

Wajuzi wa afya wanasema kuwa, unapotumia chumvi nyingi, figo hushindwa kuondoa chumvi ya ziada mwilini, na kupelekea maji kujaa mwilini. Hali hii, madaktari wanaonya, husababisha mishipa ya damu kupoteza uwezo wake wa kutanuka na kusinyaa, na kupelekea mtu kupatwa na magonjwa ya moyo, shambulizi la moyo, kiharusi, na kukuweka katika hatari ya kupatwa na saratani ya tumbo na mifupa kulegea.

Madaktari wanatoa nasaha kuwa, ili kuepukana na hatari ya magonjwa hayo, watu wenye miaka 14 na zaidi hawapasi kula zaidi ya gramu 6 ya chumvi kwa siku. Watoto huhitaji kiasi kidogo zaidi ya chumvi tofauti na watu wazima.