Raia wa Italia akataa kumfanyia Netanyahu kazi ya ukalimani
Mkalimani wa Kitaliano amekataa katakata kumfanyia kazi ya tarjumu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, na kumtaja mwanasiasa huyo kama mtu hatari.
Olga Dalia Padoa awali alikubali ombi la kazi hiyo ya ukalimani alipoombwa na ubalozi wa Israel mjini Rome, lakini baadaye akasema kuwa ameghairi msimamo wake, na hatamfanyia ukalimani Benjamin Netanyahu ambaye yuko katika safari rasmi nchini Italia.
Habari zaidi zinasema kuwa, Padoa alipasa kuwa mkalimani wa Netanyahu leo Ijumaa, ambapo kiongozi huyo Mzayuni mwenye misimamo mikali anatazamiwa kuhutubia katika hafla itakayofanyika katika Sinagogi moja mjini Rome.
Katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook, mkalimani huyo amesema: Baada ya kutafakari kwa kina, nimefikia uamuzi wa kutomfanyia kazi ya ukalimani Netanyahu, kwa kuwa si tu sikubaliani na misimamo yake ya kisiasa, lakini pia uongozi wake ambao ni hatari.
Padoa ameashiria wimbi la maandamano ya kupinga utawala wa kidikteta wa Benjamin Netanyahu na kuitaja kama harakati ya mapambano ya kiraia, na kusema kuwa mtawala huyo anakabiliwa na msururu wa kesi za ufisadi.
Maelfu ya Wazayuni jana Alkhamisi walimiminika mitaani kushiriki maandamano makubwa zaidi dhidi ya Netanyahu yaliyopewa jina la "Kupambana na Udikteta." Waandamanaji walifunga barabara kuu zinazoelekea Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion, kujaribu kumzuia Waziri Mkuu wa utawala huo asiende Italia.
Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni navyo vimeripoti kuwa, tangu jana asubuhi maandamano makubwa ya wapinzani wa Netanyahu yamefanyika katika maeneo zaidi ya 130 ya ardhi hizo za Palestina zilizopoachikwa jina bandia la Israel.