Mar 14, 2023 02:08 UTC

Taasisi ya kimataifa ya utafiti wa Amani imetangaza kuwa mwaka jana wa 2022 Ulaya ilipokea silaha maradufu; hatua inayoashiria kupatiwa Ukraine shehena kubwa ya silaha kwa kisingizio cha vita vinavyoendelea nchini humo.

Taasisi hiyo ya kimataifa ya utafiti wa amani ya Stockhom Sweden imeashiria kuingizwa silaha maradufu barani Ulaya yaani kwa kiwango cha asilimia 93 mwaka uliopita na kutangaza kuwa hatua ya kuingizwa silaha huko Ukraine kwa kisingizio cha vita vinavyoendelea nchini humo inaonyesha ongezeko la asilimia 47 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita. 

Moja ya silaha zilizoingizwa Ulaya mwaka 2022

Kwa mujibu wa ripoti ya taasisi hiyo ya kimataifa ya utafiti wa amani, vita vya Ukraine vimeongeza mahitaji ya silaha kutoka kwa baadhi ya nchi za Ulaya kama vile Poland na Norway.

Vita vya Ukraine vimeingia katika mwezi wa 13 sasa vikiwa vimesababisha taathira kubwa za kisiasa, kijeshi, kiuchumi, kijamii na hata kiutamaduni; huku nchi za Magharibi zikiendelea kutuma silaha nchini humo.  

Nchi za Ulaya na Magharibi hasa Marekani kwa kushadidisha vikwazo dhidi ya Shirikisho la Russia huku zikiipatia serikali ya Kiev silaha nyepesi na nzito za aina mbalimbali si tu hazijachukua hatua ili kuhitimisha vita huko Ukraine bali zimeendelea kuchochea moto wa vita nchini humo.  

Russia kwa upande wake imesema mara kadhaa kuwa kitendo cha nchi za Magharibi cha kutuma silaha Ukraine  kitapelekea tu kudumu kwa muda mrefu mzozo nchini humo.  

Tags