Russia: Malengo yetu Ukraine yataweza kufikiwa kwa operesheni za kijeshi tu
Msemaji wa ofisi ya rais wa Russia amesema malengo ya nchi hiyo nchini Ukraine yanaweza kufikiwa kupitia operesheni za kijeshi tu.
Dmitry Peskov, msemaji wa ofisi ya rais wa Russia alitangaza msimamo huo jana Jumanne katika mkutano na waandishi wa habari mjini Moscow na kubainisha kwamba nchi hiyo lazima ifikie malengo yake nchini Ukraine, ambayo kwa sasa, uwezekano wa kuyafanikisha ni kutumia operesheni za kijeshi tu, na kwamba Kyiv haina budi kuikubali hali halisi mpya kabla ya kufikia suluhu kwa njia ya amani.
Vita nchini Ukraine pamoja na athari zake zote za kisiasa, kijeshi, kiuchumi, kijamii na hata kiutamaduni viko katika mwezi wake wa 13, huku nchi za Magharibi zikiwa zingali zinaendelea kutuma silaha kwa Ukraine.
Hatua ya nchi za Ulaya na Magharibi, hasa Marekani, ya kuzidisha mashinikizo ya vikwazo dhidi ya Shirikisho la Russia na kuipatia kila aina ya silaha nyepesi na nzito serikali ya Kyov, sio tu haijasaidia kukomesha vita vya Ukraine, lakini pia imekoleza na kuchochea zaidi moto wa mgogoro katika nchi hiyo.
Maafisa wa Russia na baadhi ya wataalamu na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi wamevitaja vita vya Ukraine kuwa ni vita vya uwakilishi na niaba kati ya Magharibi na Russia.
Serikali ya Moscow imekuwa ikisema mara kwa mara kuwa kupelekwa silaha za nchi za Magharibi hukoUkraine kutarefusha tu mzozo katika nchi hiyo na kuwa na matokeo yasiyoweza kutabirika.../