Vassily Nebenzia: Tutafungua mahakama ya kimataifa ya uhalifu kuhusu Ukraine
https://parstoday.ir/sw/news/world-i95250-vassily_nebenzia_tutafungua_mahakama_ya_kimataifa_ya_uhalifu_kuhusu_ukraine
Balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa ametoa matamshi yake kuhusu uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu dhidi ya Rais na Kamishna wa Haki za Watoto wa Russia akisema Moscow inajiandaa kufungua kesi kuhusiana na Ukraine.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 18, 2023 10:50 UTC
  • Vassily Nebenzia
    Vassily Nebenzia

Balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa ametoa matamshi yake kuhusu uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu dhidi ya Rais na Kamishna wa Haki za Watoto wa Russia akisema Moscow inajiandaa kufungua kesi kuhusiana na Ukraine.

Vassily Nebenzia, jana Ijumaa akijibu uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu dhidi ya Rais Vladimir Putin na Kamishna wa Haki za Watoto wa Russia, Maria Lvova-Belova, alitangaza kuwa nchi hiyo inajiandaa kufungua kesi ya kimataifa kuhusu Ukraine.

Vassily Nebenzia aliongeza kuwa kuna mahakama ya kimataifa nchini Russia ambayo iko kazini sasa na inakusanya nyaraka na ushahidi.

Matamshi hayo yametolewa baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kutoa hati ya kumkamata Rais wa Russia Vladimir Putin, ikidai kuwa ni muhusika mkuu wa uhalifu wa kivita nchini Ukraine. Ikulu ya Rais wa Russia, Kremlin imepuuzilia mbali hati hiyo na kuitaja kuwa batili. Imesisitiza kuwa ICC haina mamlaka ya kisheria.

Russia imekanusha madai hayo ikisema uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ni wa kidhalimu, usio na thamani wala maana yoyote.

Akitoa tamko kuhusu kadhia hiyo, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema Moscow haitambui mamlaka ya ICC. Amesema maswali yaliyoibuliwa na mahakama ni "ya kuchukiza na yasiyokubalika", na kusisitiza kuwa maamuzi yoyote ya mahakama hiyo ni "batili na yasiyofaa" kwa hadhi ya Russia.

Dmitry Peskov

Naye msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Russia Maria Zakharova amesema kuwa waranti hiyo haina maana yoyote.

Tarehe 24 Februari mwaka uliomalizika 2022, Rais Vladimir Putin wa Russia alitoa amri ya kuanza operesheni maalumu ya kijeshi katika eneo la Donbass, akijibu ombi la msaada wa kijeshi kutoka kwa Marais wa Jamhuri za Donetsk na Luhansk.

Hatua hiyo ya Putin ilichukuliwa sanjari na hatua ya Ukraine ya kutaka kujiunga na Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (NATO) ambao ni tishio kwa Russia.