Waislamu Indonesia walaani uepo wa Israel Kombe la Dunia U20
(last modified Tue, 21 Mar 2023 02:28:43 GMT )
Mar 21, 2023 02:28 UTC
  • Waislamu Indonesia walaani uepo wa Israel Kombe la Dunia U20

Wananchi Waislamu wa Indonesia wamefanya maandamano ya kulalamikia hatua ya kuruhusiwa utawala haramu wa Israel kushiriki katika fainali za Kombe la Dunia katika mchezo wa kandanda kwa vijana wa kiume wenye umri usiozidi miaka 20.

Waandamanaji hao katika mji mkuu wa Indonesia, Jakarta wamesema Israel inapasa kuondolewa kwenye mashindano hayo ya kimataifa ambayo yataandaliwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kuanzia Mei 20 hadi Juni 11 mwaka huu 2023. 

Nchi 23 pamoja na utawala pandikizi wa Israel zinatazamiwa kushiriki kwenye michuano hiyo itakayopigwa katika miji sita ya Indonesia. Mashindano hayo yaliakhirishwa kwa miaka miwili kutokana na janga la kimataifa la Corona.

Ingawaje Indonesia haina uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel na ni muungaji mkono mkubwa wa Palestina, lakini serikali ya Jakarta imesema haitauzuia utawala huo wa Kizayuni kushiriki kwenye mashindano hayo. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa utawala huo unaoua watoto wa Kipalestina kushiriki kwenye mashindano hayo ya FIFA. 

Sambamba na kuonyesha uungaji mkono wao kwa Wapalestina, waandamanaji hao katika mji mkuu Jakarta walisikika wakipiga nara za 'Allahu Akbar' huku wakitaka kuondolewa Israel kwenye mashindano hayo ya soka ya Under 20.

Palestina, mshindi halisi wa Kombe la Dunia Qatar 2022

Si vibaya kuashiria hapa kuwa, moja ya matukio ya kuvutia katika mashindano ya soka ya Kombe la Dunia yaliyofanyika huko Qatar mwishoni mwaka uliopita 2022 ni kitendo cha watazamaji kutoka nchi mbalimbali kuiunga mkono Palestina mkabala wa utawala wa Kizayuni.

Aidha katika duru ya saba ya mashindano ya soka ya Mataifa ya Afrika (CHAN) kwa wachezaji wa ligi za ndani barani humo mapema mwaka huu, mashabiki walisikika wakipaza sauti kuliunga mkono taifa la Palestina linalokandamizwa na utawala haramu wa Israel kwa uungaji mkono wa Marekani na washirika wake.