Kuendelea kudhoofika sarafu ya dola ya Marekani
Mazungumzo baina ya Muungano wa Kiuchumi wa Eurasia (EAEU) na India yameanza kwa shabaha ya kuanzisha eneo huru la biashara. Maana ya hatua hiyo ni kuzidi kuporomoka nguvu za sarafu ya dola ya Marekani, duniani.
Denis Manturov, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Russia amesema wakati huu wa kukaribia kikao cha 24 cha kamisheni ya pamoja ya Russia na India kwamba lengo la Muungano wa Kiuchumi wa Eurasia (EAEU) ni kuanzisha eneo huru la pamoja la kibiashara kwa kuishikisha pia India. Amesema, kumewekwa mipango mizuri na maalumu ya kuhakikisha kuwa mabadilishano ya kibiashara baina ya pande hizo mbili yanatumia fedha za mataifa husika na si dola ya Marekani. Ameongeza kuwa, Russia inalipa umuhimu wa kipekee suala la kila nchi kupewa uhuru kamili wa kuingia katika masoko ya kimataifa na ina matumaini, kwa kupitia kamisheni ya kiuchumi ya Eurasia, mazungumzo ya kamisheni hiyo na India yatakuwa ya mafanikio na kutapatikana maafikiano ya haraka baina ya pande mbili.
Ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba kuanzishwa eneo huru la kibiashara baina ya India na Eurasia, ni sehemu ya njia za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi baina ya pande mbili. Ushirikiano huo ni muhimu sana hivi sasa, hasa baada ya nchi mbili za India na Russia kuanzisha kampeni ya kutumia fedha zao za taifa katika miamala yao na kuipiga teke sarafu ya dola katika mabadilishano yao ya kibiashara. Tuelewe pia kuwa nchi zote duniani zinatambua kwamba, sarafu ya dola ni moja ya silaha kubwa zinazotumiwa na wanasiasa wa Marekani kufanikishia malengo yao ya kibeberu na kuzikandamiza nchi nyingine duniani. Viongozi wa Marekani wana ugonjwa na uraibu mkubwa wa kuziwekea vikwazo kiholela nchi nyingine kwa kutumia nguvu za sarafu ya dola. Sababu yake ni kwamba, njama za Marekani za kutumia mabavu ya kijeshi kufanikisha malengo yake ya kiistikbari zimefeli na ndio maana wakuu wa White House wameamua kutumia vikwazo vya kiuchumi dhidi ya mahasimu wao badala ya kutumia nguvu za kijeshi.
Ni wazi kwamba, vikwazo vya Marekani haviwezi kuwa na taathira yoyote iwapo nchi huru duniani zitaipiga teke sarafu ya dola na kutumia fedha za mataifa yao katika mabadilishano ya kibiashara. Ni kwa sababu hiyo ndio maana nchi nyingi za ukanda huu na duniani kiujumla kama vile Iran, Russia, India, Uturuki, China na nchi nyingine duniani, zimechukua hatua za kuipiga teke sarafu ya dola na kutumia sarafu za mataifa yao.
Miongoni mwa pigo kubwa iliyopata sarafu ya dola ni uamuzi wa jumuiya kubwa ya kiuchumi ya nchi zinazostawi kwa kasi yaani jumuiya ya Brics. Kambi hiyo ya kiuchumi imeamua kuweka akiba zake za fedha za kigeni kwa sarafu nyingine na si dola ya Marekani. Wakati huo huo Benki Kuu ya Indonesia imeungana na nchi nyingine wanachama wa jumuiya ya Brics kuendesha kampeni ya kuitoa sarafu ya dola katika miamala yake ya kiuchumi na kibiashara. Kabla ya hapo tayari Indonesia ilikuwa ikifanya miamala ya kibiashara na nchi kama Thailand, Malaysia, China na Japan kwa kutumia sarafu nyingine, si dola ya Marekani. Sasa hivi inakusudia kuipiga teke jingine dola ya Marekani katika miamala yake ya kiuchumi na kibiashara na Korea Kusini.
Jumuiya ya Brics inaundwa na nchi za Brazil, China, Russia, Afrika Kusini na Indonesia. Nchi hizo hivi sasa zimeafikiana kutotumia sarafu ya dola katika miamala na mabadilishano yao ya kiuchumi na kibiashara. Nchi hizo zimekusudia kikwelikweli kutumia fedha za mataifa yao katika miamala hiyo. Kwa hakika nchi huru duniani zimetambua kuwa, zitazidi kudhoofika kadiri zinavyoendelea kutumia sarafu ya dola katika miamala yao na katika upande wa pili, zitazidi kuchangia kuimarika uchumi wa Marekani kwa kutumia kwao sarafu ya dola. Hivyo zimeamua kuanzisha kampeni maalumu ya kuachana kabisa ya sarafu ya dola katika miamala yao.