Kuendelea chuki dhidi ya Uislamu zinazofanywa na serikali ya India
https://parstoday.ir/sw/news/world-i96700-kuendelea_chuki_dhidi_ya_uislamu_zinazofanywa_na_serikali_ya_india
Serikali ya India yenye misimamo ya kufurutu ada imefuta historia ya watawala wa Kiislamu katika vitabu vya masomo na kuzidi kuthibitisha kwamba, inafuatilia kwa nguvu zote siasa za kukabiliana na Waislamu pamoja na historia yao.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Apr 26, 2023 21:42 UTC
  • Kuendelea chuki dhidi ya Uislamu zinazofanywa na serikali ya India

Serikali ya India yenye misimamo ya kufurutu ada imefuta historia ya watawala wa Kiislamu katika vitabu vya masomo na kuzidi kuthibitisha kwamba, inafuatilia kwa nguvu zote siasa za kukabiliana na Waislamu pamoja na historia yao.

Baada ya Waziri Mkuu Narendra Modi mwenye mielekeo ya kihindu kushika hatamu za uongozi nchini India siasa za chuki dhidi ya Uislamu za serikali ya New Delhi zilishika kasi na kuchukua wigo mpana zaidi. Mwenendo huo umeongezeka mno kiasi kwamba, Wahindu wenye misimamo ya kufurutu ada wamekuwa wakivamia na kushambulia misikiti na nembo za Kiislamu bila ya woga wowote ule. Katika mlongongo huo, hivi karibuni Wahindu wenye misimamo mikali walichoma moto maktaba ya kihistoria ya Waislamu katika jimbo la Bihar ambayo ina ukongwe wa miaka 113.

Hii ina maana kwamba, pamoja na hatua za kimaonyesho za Waziri Mkuu Narendra Modi za kushirikiana na Waislmau, lakini Wahindu ambao wanaungwa mkono na serikali yake ya chama tawala cha Bharatiya Janata (BJP) wanaendelea kutenda jinai zao dhidi ya Waislamu. Rajiya Singh, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema kuhusiana na hili kwamba:

Vyama vyenye misimamo mikali na ya kufurutu ada vya India kama RSS na Shiv Sena vina himaya na uungaji mkono kamili wa serikali ya India na ndio maana vimekuwa vikifanya kila jinai dhidi ya Waislamu na kutokuwa na wasiwasi wowote. Viongozi wa Kiislamu nchini India wametahadharishha mara chungu nzima katika mazungumzo yao na viongozi wa serikali ya New Delhi kuhusiana na matokeo mabaya ya vitendo vya Wahindu vya kuvunjia heshima nembo za Kiislamu sambamba na hujuma dhidi ya wafuasi wa dini hii.

 

Pamoja na hayo, kufutwa historia ya Waislamu katika vitabu vya masomo vya India ni hatua inayoonyesha ni kwa kiasi gani chuki dhidi ya Uislamu zinavyofanywa na serikali ya India zimechukua wigo mpana tena kwa sura rasmi. Baraza la Taifa la Uhakiki wa Malezi na Masomo la India lenye jukumu la kuandaa mitaala na rariba za masomo ya shule na vituo vya elimu, limechukua hatua ya kufuta faslu na milango inayohusiana na historia ya watawala wa Kiislamu katika karne ya 19 nchini humo na kuiondoa kabisa katika vitabu vya masomo.

Hii inaonyesha kuwa, Wahindu wenye misimamo ya kufurutu ada ambao wanashikilia nafasi za juu kabisa serikalini wanafuatilia kwa hali na mali mipango yao ya kufuta athari zozote zile zinazohusiana na Waislamu katika historia ya nchi hiyo. Hii ni kutokana na kuwa, Baraza la Malenzi na Masomo la India ambalo lina mfungamano na Wizara ya Elimu ya nchi hiyo linadhibitiwa na chama tawala cha Bharatiya Janata.

Ukweli wa mambo ni kuwa, chama hiki kikiwa na lengo la kuwaridhisha Wahindu hususan makundi yenye kufurutu ada, kimekuwa kikifanya kila kiwezalo kuwaandama Waislamu.

Msikiti wa Babri ulishambuliwa na kubomolewa na Wahindu wenye misimamo ya kufurudu ada kwa uungaji mkono wa chama tawala cha Bharatiya Janata (BJP) mnamo mwezi Disemba 1992. Zaidi ya Waislamu 2000 waliuawa katika hujuma hiyo.

 

Alaa kulli haal, kuchomwa maktaba iliyokuwa na vitabu 4,500 vyenye thamani kubwa ni hatua inayoonyesha chuki kuubwa waliyonayo Wahindu wenye misimamo mikali dhidi ya Waislamu, ambapo serikali ya India  inapaswa kubeba dhima matokeo yake. Katika miaka ya hivi karibuni Wahindu wamechukua hatua chungu nzima dhidi ya Waislamu kama kuhujumu misikiti na kuichoma moto.

Mwenendo wa chuki dhidi ya Uislamu wa chama tawala cha Bharatiya Janata ulianza kushika kasi mwaka 2019 kwa kuifutia Kashmir mamlaka maalumu ya kujitawala. Aidha katika miaka ya hivi karibuni, chuki dhidi ya Waislamu nchini India zimeshtadi hasa baada ya Bunge la nchi hiyo kupasisha marekebisho ya sheria ya uraia ambayo yanawapa haki ya uraia wahajiri wasio Waislamu wanaolazimika kuhama nchi jirani za Bangladesh, Pakistan na Afghanistan na kuhamia India; lakini haki hiyo haiwahusu wahajiri kutoka nchi hizo ambao watakuwa ni Waislamu.