$206m zatumika kueneza hofu na chuki dhidi ya Uislamu Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i9700-206m_zatumika_kueneza_hofu_na_chuki_dhidi_ya_uislamu_marekani
Imebainika kuwa kueneza chuki na woga dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini Marekani kumegeuzwa kuwa biashara yenye kugharimu mamilioni ya dola za nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 21, 2016 23:35 UTC
  • $206m zatumika kueneza hofu na chuki dhidi ya Uislamu Marekani

Imebainika kuwa kueneza chuki na woga dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini Marekani kumegeuzwa kuwa biashara yenye kugharimu mamilioni ya dola za nchi hiyo.

Ripoti mpya ya Baraza la Mahusiano ya Kiislamu na Marekani (CAIR) kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Berkeley jimboni California imefichua kuwa, mashirika yapatayo 74 yametoa kiasi cha dola milioni 206 za Marekani kwa ajili ya kutumika kueneza chuki na hofu dhidi ya Uislamu nchini humo.

Corey Saylor, mwandishi wa ripoti hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Kupambana na Chuki dhidi ya Uislamu iliyo chini ya Baraza la Mahusiano ya Kiislamu na Marekani (CAIR) kampeni za mashirika hayo zimekuwa na taathira hasi nchini humo na kwamba baadhi ya athari zake ni kuchomwa moto baadhi ya misikiti katika kona mbalimbali ya nchi sambamba na kushawishi kubuniwa sheria kali dhidi ya wafuasi wa dini hiyo nchini Marekani.

Mashirika hayo ni pamoja na Abstraction Fund, Clarion Project, David Horowitz Freedom Center, Middle East Forum, American Freedom Law Center, Center for Security Policy, Investigative Project on Terrorism, Jihad Watch na Act for America, ambayo yalitoa mamilioni ya dola za nchi hiyo katika kipindi cha kati ya mwaka 2008 na 2013 ili zitumike kueneza chuki dhidi ya Uislamu na wafuasi wake nchini humo.

Sanjari na kushika kasi kampeni za uchaguzi wa rais nchini Marekani, suala la chuki na ubaguzi dhidi ya Uislamu na Waislamu limeongezeka mara dufu, huku baadhi ya wanasiasa kama vile mgombea wa kiti cha rais wa chama cha Republican, Donald Trump wakitoa wazi wazi maneno makali dhidi ya wafuasi wa dini hiyo tukufu.