Uchaguzi Mkuu wa Mei 14 nchini Uturuki na ahadi za wanasiasa
Ahadi za kila namna za wanasiasa zimepamba moto hivi sasa katika wakati huu wa kukaribia chaguzi mbili muhimu mno na za wakati mmoja za rais na bunge nchini Uturuki.
Katika uchaguzi wa Mei 14 mwaka huu nchini Uturuki, vyama 13 huru vya kisiasa vitashiriki na vyama vingine 13 vitashiriki chini ya mwavuli wa miungano ya aina nne. Baadhi ya vyama vya siasa vinashiriki katika uchaguzi ujao nchini Uturuki katika mfumo wa miungano mitano tofauti inayoitwa "Muungano wa Jamhuri," "Muungano wa Taifa," "Muungano wa ATA," "Muungano wa Kazi na Uhuruu," na "Muungano wa Nguvu za Kisoshalisti." Rais Recep Tayyip Erdoğan ni mgombea wa chama tawala na Muungano wa Jamhuri. Si tu katika kamopeni zake anadai uhuru wa Uturuki katika masuala ya nishati, lakini pia ameitangaza Uturuki kuwa muuzaji mwingine wa nishati ulimwenguni.
Kwa kweli, tunalazimika kusema kwamba, Erdogan amejipanga vizuri sana kuhakikisha anashindwa tena katika uchaguzi wa Mei 14. Hivi karibuni alitangaza kugunduliwa kisima cha mafuta chenye uwezo wa kuzalisha mapipa laki moja kwa siku katika eneo la "Gabar" katika sherehe za ufunguzi wa miradi kadhaa, ikiwa ni pamoja na kiwanda cha kuzalisha nishati ya jua cha "Karapinar" na bwawa la "Bozker" huko Konya. Katika sehemu moja ya hotuba yake Erdoğan aliahidi kutokomeza ugaidi nchini Uturuki na kusema, "Tutaondoa kila kikwazo kinachokwamisha juhudi zetu za kustafidi na utajiri wa maliasi wa nchi yetu." Vile vile ametangaza kuwa, matatizo ya kiuchumi ya wananchi yataweza kutatuliwa ikiwa miradi ya mafuta na gesi itakamilika na kutumika vizuri.
Kauli na ahadi hizo za Recep Tayyip Erdoğan zinaonesha kuwa, tegemeo pekee la chama tawala nchini Uturuki ni kutoa ahadi za kiuchumi za kuboresha hali ya maisha kwa wananchi. Ahadi hizo zimetolewa baada ya serikali ya Ankara kujiondoa katika siasa za mivutano na majirani zake na nchi za eneo na dunia kwa ujuumla. Lakini bado viongozi wa chama tawala cha Muungano wa Jamhuri huko Uturuki, hawajatoa maelezo ya kuridhisha kuhusu namna ya kupitishwa sera hizo na sababu zilizopelekea Uturuki kukumbwa na mzozo wa kiuchumi na matatizo ya maisha ya wananchi wake.
Ukweli ni kwamba sera za kutumia mabavu ya kijeshi za serikali ya Recep Tayyip Erdoğan, ndiyo sababu ya matatizo iliyo nayo Uturuki hivi sasa. Maafisa wa Ankara hivi karibuni wametangaza kuwa wameingia katika mazungumzo ya amani na Syria baada ya miaka mitano ya kutumia mabavu ya kijeshi kwa tamaa ya kuipindua serikali ya Damascus. Lakini Rais Bashar al Assad wa Syria amesema wazi kwamba kuondolewa wanajeshi wa Uturuki ndani ya ardhi ya Syria ndilo sharti la kwanza la mazungumzo yoyote na viongozi wa Ankara. Hata hivyo,wataalamu na wachambuzi wa vyombo vya habari wa Uturuki walikuwa wanasema kuwa, mbinu kuu iliyotegemewa na Recep Tayyip Erdoğan kwa ajili ya kupata ushindi katika uchaguzi ujao ni kutoa maneno makali na kuwashambulia vila ya huruma wapinzani wake hasa Kemal Kılıçdaroğlu, ambaye anahesabiwa ni mtu mwenye misimamo yua wastani na mwenye maadili mazuri. Lakini hivi sasa na kwa sababu mbalimbali, inaonekana Erdogan ameachana na siasa hizo na hivi sasa anaishia tu kuwatuhumu wapinzani wake. Kwa upande wake, Kemal Kılıçdaroğlu, mkuu wa Chama cha Jamhuri ya Watu na mgombea wa Muungano wa Taifa, na ambaye hivi karibuni alipata uungaji mkono wa makundi ya Wakurdi, anajaribu kujikusanyia kura nyingi kwa ahadi zake kwa wapiga kura. Mpinzani huyo mkubwa wa Erdogan katika uchaguzi wa Mei 14, anazungumzia ramani ya njia yenye nukta 7 za kuukwamua uchumi wa Uturuki. Kwa mujibu wa mgombea huyo, mpango wake huo utaweza kukabiliana na mgogoro mkubwa wa kiuchumi na utatatua matatizo ya kimaisha ya watu wa Uturuki. Ahadi zake nyingine na kurejesha hali ya uaminifu na utawala wa sheria kwa Uturuki nzima akisema kuwa hiyo ni mojawapo ya njia bora za kutatua matatizo ya hivi sasa ya Uturuki.
Akihojiwa na gazeti la "Financial Times" mwishoni mwa mwezi uliopita wa Aprili, Kemal Kılıçdaroğlu alitoa ahadi akisema: "Nitahakikisha Uturuki inajiunga na Umoja wa Ulaya haraka iwezekanavyo, iwapo nitashinda katika uchaguzi huo. Kuboreshwa hali ya uchumi ya Uturuki ni ahadi nyingine wa mgombea wa Muungano wa Taifa. Wakati huo huo kambi ya upinzani imeishutumu kambi ya chama tawala kwa kutumia suhula za serikali kwa manufaa ya Erdoğan katika uchaguzi ujao na tayari wamezungumzia suala la chama tawala na waziri wa mambo ya ndani wa Uturuki kujaribu kufanya udanganyifua na uchakachuaji wa matokeo ya uchaguzi huo.
Kiujumla ni kwamba, kwa hivi sasa ni vigumu kutabiri kuwa mpinzani wa Erdogan anaweza kushinda uchaguzi wa Mei 14 nchini Uturuki hasa kwa kuzingatia matokeo ya uchunguzi mbalimbali wa maoni ya wananchi uliofanywa na vyombo vya habari kwa nyakati tofauti. Utabiri pekee ambao unaweza kutolewa kwa manufaa ya wapinzani, ni kuingia uchaguzi huo katika duru ya pili. Wachambuzi wengine wa masuala ya siasa za Uturuki wanasema kuwa, iwapo wagombea wengine wawili yaani "Moharrem Ince" na "Sinan Ogan" watajiondoa hasa kwa vile wana nafasi ndogo zaidi ya kushinda katika uchaguzi ujao basi kura za Kemal Kılıçdaroğlu zitaongezeka na zinaweza hata kumpa ushindi na kumpiga kikumbo Erdogan katika uchaguzi huo wa Mei 14.