Gharama za kijeshi za Umoja wa Ulaya zimeongezeka kwa asilimia 30
(last modified Sun, 14 May 2023 11:35:35 GMT )
May 14, 2023 11:35 UTC
  • Gharama za kijeshi za Umoja wa Ulaya zimeongezeka kwa asilimia 30

Mkuu wa Sera za Nje za Umoja wa Ulaya Josep Borrell ametangaza kuwa gharama za kijeshi za umoja huo zimeongezeka kwa asilimia 30.

Borrell ameyasema hayo katika ufunguzi wa kongamano la mawaziri wa nchi za umoja huo na za maeneo ya Bahari ya Hindi na Pasifiki lililofanyika katika mji mkuu wa Sweden, Stockholm na akabainisha kuwa gharama za kijeshi za Umoja wa Ulaya zimeongezeka kwa asilimia 30 tangu mwaka 2014.

Hayo yanaripotiwa huku Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI) ikitangaza kuwa chimbuko la ongezeko la gharama za fedha katika uga wa kijeshi kwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya katika mwaka 2022 limetokana na vita vya Ukraine; na wataalamu wengi pamoja na waangalizi wa kimataifa wanaamini kuwa ung'ang'anizi wa Magharibi hasa Marekani wa kupanua wigo wa satua za shirika la kijeshi la NATO ndio uliosababisha hali hiyo.

Wakati huo huo, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine, jana usiku aliwasili Berlin, mji mkuu wa Ujerumani kwa kisingizio cha kwenda kupokea silaha kwa ajili ya vita kati ya nchi yake na Russia, wakati siku moja kabla ya kuwasili kiongozi huyo maandamano makubwa ya kupinga vita yalifanyika huko Hanover, Ujerumani. Waandamanaji walitoa nara za "ni diplomasia badala ya utumaji silaha!" na "tunataka amani".

Kwa kisingizio cha vita vya Ukraine, serikali ya Berlin leo inatazamiwa kuipatia Kiev silaha zaidi zenye thamani ya yuro bilioni 2.7 (takriban dola bilioni 3) huko mjini Aachen nchini Ujerumani.

 

Jana Jumamosi, Zelensky alikutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis mjini Vatican, ambapo alilikataa tena pendekezo la kiongozi huyo wa kidini la kufanya usuluhishi wa kuhitimisha vita vya Ukraine.

Pamoja na athari zake zote hasi za kisiasa, kijeshi, kiuchumi, kijamii na hata kiutamaduni, vita vya Ukraine hivi sasa viko katika mwezi wake wa 15, huku nchi za Magharibi zikiendelea kutuma aina mbalimbali ya silaha kwa serikali ya Kiev.../

Tags