Kremlin yajibu vitisho vya Ukraine vya kumuua Rais wa Russia
Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Russia (Kremlin) amesema hatua ya watawala wa Ukraine ya kutishia kumuua kigaidi Rais Vladimir Putin wa Russia imeonyesha dhati ya ugaidi ya viongozi wa Kiev.
Dmitry Peskov alisema hayo jana Alkhamisi na kusisitiza kuwa, vyombo vya usalama vya Russia vinajua vizuri kazi yao ya kumdhaminia usalama kiongozi wa nchi hiyo.
Kauli ya Peskov ni jibu kwa matamshi ya Vadim Skibitsky, Naibu Mkuu wa Idara ya Intelijensia ya Ukraine ambaye aliliambia shirika la habari la Ujerumani la Die Welt juzi Jumatano kuwa, Putin yupo katika orodha ya watu wanaowindwa na idara hiyo ili wauawe.
Msemaji wa Ikulu ya Rais wa Russia ameeleza bayana kuwa, matamshi kama hayo yanaonesha kuwa operesheni ya kijeshi ya Russia dhidi ya Ukraine iliyoanza Februari 2022 inahalalishika, ni ya dharura na inapaswa kuendelea hadi tamati.
Ikumbukwe kuwa, mapema mwezi huu wa Mei, kulijiri shambulio la ndege isiyo na rubani (droni) dhidi ya Ikulu ya Rais wa Russia. Hata hivyo Putin hakuwepo ndaniya Kremlin wakati wa shambulio hilo lililofeli.
Video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ya Russia, ikiwa ni pamoja na mtandao wa kijamii wa Telegram ya chombo cha habari cha kijeshi Zvezda, ilionyesha moshi mweupe nyuma ya jumba kuu la Kremlin baada ya tukio hilo.
Baada ya hujuma hiyo, Dmitry Medvedev, Naibu wa Mkuu wa Baraza la Usalama la Russia alitoa wito wa kuuawa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky.