Raia milioni 3.5 wa Ukraine wamekimbilia Russia tokea Februari 2022
https://parstoday.ir/sw/news/world-i98106-raia_milioni_3.5_wa_ukraine_wamekimbilia_russia_tokea_februari_2022
Zaidi ya raia milioni tatu na laki tano wa Ukraine wametorokea nchini Russia tangu operesheni ya kijeshi ya Moscow dhidi ya Kiev ianze mnamo Februari 2022.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 28, 2023 03:05 UTC
  • Raia milioni 3.5 wa Ukraine wamekimbilia Russia tokea Februari 2022

Zaidi ya raia milioni tatu na laki tano wa Ukraine wametorokea nchini Russia tangu operesheni ya kijeshi ya Moscow dhidi ya Kiev ianze mnamo Februari 2022.

Hayo yamesemwa na Vladimir Kulishov, Mkuu wa Idara ya Gadi ya Mpakani ya Russia na kuongeza kuwa, serikali ya Moscow imechukua hatua kadhaa za kufanikisha mchakato wa kuwapokea mamilioni ya raia wa Ukraine walioamua kukimbilia nchini Russia.

Kulishov ameliambia shirika la habari la Russia la TASS kuwa, mgogoro huo wa wakimbizi umeshtadi kutokana na hatua za kichokozi za Kiev katika mpaka wa nchi hizo mbili.

Februari 21, 2022, Rais wa Russia alikosoa mienendo ya nchi za Magharibi ya kupuuza wasiwasi wa usalama wa Moscow na akatangaza kutambua rasmi uhuru wa Jamhuri za Watu wa Donetsk na Luhansk katika mkoa wa Donbas huko Ukraine.

Siku tatu baadaye, Februari 24, 2022, Putin alianzisha operesheni "maalumu ya kijeshi" dhidi ya Ukraine, na vita baina ya pande hizo mbili bado vinaendelea. Maelfu wameuawa na kujeruhiwa, mbali na mamilioni kulazimika kuwa wakimbizi.

TASS iliripoti mwezi Machi mwaka huu kwamba, idadi ya wakimbizi wa Ukraine katika eneo la Donbass la Russia imepindukia watu milioni 5.4, wakiwemo watoto 744,000.

Nchi za Ulaya zinakadiriwa kupokea wakimbizi karibu milioni nne kutoka Ukraine, tangu mapigano hayo yaanze mnamo Februari mwaka jana.