Uzushi na undumakuwili wa Zelensky dhidi ya Iran
Rais wa Ukraine kwa mara nyingine tena ameitaka Iran isiipatie Russia ndege za kivita zisizo na rubani kauli ambayo ameitoa kwa kutegemea madai bandia ambayo yamepingwa mara kadhaa na Iran na pia Ukraine haijaweza kutoa ushahidi wowote wa maana kuhusu madai hayo.
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine, katika onyesho jipya la propaganda, lenye kutegemea tuhuma ambazo zimekanushwa mara nyingi na Tehran, amewataka wananchi wa Iran kutoegemea upande wa Russia na kwamba eti wasiwe upande mbaya wa historia.
Akiendelea na madai yake, Zelensky amehoji kwa kusema, ni kwa nini ,mnataka kuwa washiriki katika vitendo vya kigaidi vya Russia? Katika ujumbe wake wa video, amewataka wananchi wote wa Iran kuathiri uamuzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran eti wa kutuma ndege zisizo na rubani nchini Russia ili wasiwe katika upande mbaya wa historia na wasishiriki katika kile kinachoitwa ugaidi na vitisho vya Russia.
Katika kujibu kauli ya Zelenskiy, Nasser Kanani Chafi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, amesema kuwa madai ya uongo ya rais wa Ukraine yanalenga kuvutia msaada wa silaha za Magharibi.
Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje amesema: "Kukaririwa madai ya uongo ya Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine dhidi ya Iran ni kuafikiana na propaganda na vita vya vyombo vya habari vya mhimili unaopinga Iran na watu wake na kunafanyika kwa lengo la kupata misaada ya silaha na fedha kutoka nchi za Magharibi." Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ametaja kauli ya Rais wa Ukraine dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni uzushi wa kupotosha fikra za umma na mchezo wa kuigiza wa kisiasa unaoandamana na madai yasiyo na msingi. Kan'ani ameongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikitangaza kuwa inapinga vita vya Ukraine na inasikitika sana kutokana na machungu na mateso ya wananchi wa Ukraine; vilevile inasisitiza ulazima wa kupatikana suluhisho la kisiasa la kukomesha vita hivyo haraka iwezekanavyo.
Ukraine na baadhi ya nchi za Magharibi ikiwemo Marekani zimedai katika miezi kadhaa iliyopita kuwa Iran imeipatia Russia ndege zisizo na rubani aina ya Shahid 131 na 136 kwa ajili ya kutumika katika vita vya Ukraine.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekanusha mara kwa mara madai hayo. Tehran imetangaza kuwa ina msimamo wa kutoegemea upande wowote katika vita hivyo, inapinga vita na inataka kusitishwa mapigano sambamba na kurejeswa amani nchini Ukraine. Wakati huo huo, tangu kuanza kwa vita vya Ukraine, Iran imesisitiza haja ya Russia na Ukraine kufikia suluhu la kisiasa ili kutatua hitilafu na kufanyika mazungumzo katika uwanja huo.
Bila shaka, Tehran pia imechukua hatua za kivitendo katika uwanja huo. Kuhusiana na suala hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amirabdollahian alikutana na maafisa wakuu wa Russia akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Sergey Lavrov katika muktadha wa vita vya Ukraine na upatanishi wa Tehran, katika safari ya Moscow iliyofanyika mwishoni mwa Agosti mwaka uliopita. Safari hii ilifanyika kufuatia ombi la Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kwa Rais Seyed Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, aliyeiomba Iran iwe mpatanishi kuhusu vita vya Russia dhidi ya Ukraine.
Pia tarehe 25 Aprili 2023, katika kikao cha Martin Griffiths, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, mjini Tehran, Amir Abdollahian alisema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitoi usaidizi wa kijeshi kwa upande wowote katika vita vya Ukraine na wala haizingatii vita kama suluhu, na kuwa inaunga mkono uhuru na mamlaka ya kujitawala nchi zote, ikiwa ni pamoja na Ukraine.
Licha ya nia njema ya Iran na juhudi zake za kumaliza vita vya Ukraine, Wamagharibi pamoja na serikali inayounga mkono Magharibi ya Kiev, wameanzisha kampeni ya kipropaganda dhidi ya Tehran, wakidai kuwepo ushirikiano wa silaha kati ya Iran na Russia, hasa madai kuwa Iran imeipa Russia idadi kubwa ya ndege za kivita zisizo na rubani. Kutokana na madai hayo yasiyo na msingi, mwishoni mwa Septemba 2022, na kufuatia kitendo kisicho cha kirafiki, Ukraine ilimtaka balozi wa Iran aondoke Kiev sambamba na kupunguza idadi kubwa ya wanadiplomasaia wa Iran nchini humo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Amir Abdollahian akijibu tuhuma dhidi ya Iran alitangaza bayana kuwa, idadi ndogo ya ndege zisizo na rubani za Iran zilikabidhiwa Russia kabla ya kuanza vita nchini Ukraine. Kwa msingi huo alisisitiza kuwa Iran haijaingilia kwa vyovyote vile vita vya Ukraine kwa manufaa ya Russia.
Wakati huo huo madai ya Kiev kuhusu matumizi ya ndege zisizo na rubani za Iran katika vita vya Ukraine yamekuwa kisingizio cha nchi za Magharibi kuweka vikwazo vipya dhidi ya Iran. Kuhusiana na hilo, Umoja wa Ulaya na Marekani zimetangaza vikwazo vipya kwa kuzingatia madai ambayo hayajathibitishwa kuhusu matumizi ya ndege zisizo na rubani zilizotengenezwa na Iran katika vita vya Ukraine.
Suala muhimu ambalo linapaswa kuzingatiwa katika muktadha wa tuhuma mpya za Zelensky ni hili kuwa je, ni kwa nini hakulalamika wala kuikosoa Marekani ilipoamua kuiwekea Iran vikwazo vya kidhalimu na visivyo vya kibinadamu, hasa tangu kipindi cha urais wa Donald Trump, baada ya Washington kujitoa katika mkataba wa nyuklia wa kimataifa wa JCPOA mwaka 2018?
Mtu anapaswa kumuuliza Zelensky yuko wapi sasa ambapo anatakiwa kuwataka watu wa Marekani wasiwe katika upande mbaya wa historia na wasiwe washiriki wa ugaidi na vitisho vya nchi hiyo dhidi ya taifa la Iran? Kwa hakika Rais wa Ukraine siku zote amekuwa mtetezi wa sera na vitendo vya kibeberu vya Marekani dhidi ya Iran ili kuvutia uungaji mkono wa Washington upande wake.