Kuinusuru Uturuki na kuendelea ukoloni wa Umoja wa Ulaya
(last modified Thu, 08 Jun 2023 06:52:21 GMT )
Jun 08, 2023 06:52 UTC
  • Kuinusuru Uturuki na kuendelea ukoloni wa Umoja wa Ulaya

Bunge la Ulaya limesema Rais Recep Tayyeb Erdogan wa Uturuki kupata fursa nyingine ya kuiongoza nchi hiyo ya Kiislamu kutakwamisha juhudi za kujiunga nchi hiyo na Umoja wa Ulaya.

Bunge la Ulaya limesema katika taarifa kuwa: "Mchakato wa kujiunga Uturuki na umoja huu ulikuwa umeshindwa kuendelea hata kabla ya uchaguzi na kutangazwa matokeo yake. Hii ni kwa sababu, mabadiliko ya msingi yalipasa kutekelezwa huko Uturuki ili mchakato huo uweze kuendelea, na bila shaka kuendelea mchakato ambao hauendani na mageuzi yanayotakiwa kutakuwa na taathira hasi." 

Kwa mujibu wa ripoti ya Bunge la Ulaya, taasisi hiyo inaamini kuhusu uhusiano wake na serikali ya Ankara kwamba, mchakato wa kujiunga Uturuki na Umoja wa Ulaya 'umefungwa na kusimamishwa' na kwamba mchakato mwingine mbadala unapasa kutafutwa.  

Katika muongo mmoja uliopita, hatua ya serikali ya Ankara chini ya uongozi wa Recep Tayyep Erdogan ya kutekeleza sera huru mkabala wa serikali za Magharibi imezitia wasiwasi na kutoziridhisha Marekani na Umoja wa Ulaya. Katika miongo kadhaa ya karibuni serikali za Magharibi zimeiweka Uturuki katika hali isiyofahamika vyema ya kusubiri kupewa uanachama katika Umoja wa Ulaya na kuitaka ishirikiane nazo katika hali hiyo, jambo ambalo limeiletea matatizo mengi. 

Rais Recep Tayyep Erdogan wa Uturuki 

Mchakato wa kujiunga Uturuki na Umoja wa Ulaya na hasa katika miongo kadhaa ya karibuni umekabiliwa na vizuizi na ucheleweshaji mkubwa. Suala hilo hatimaye  liliipelekea serikali ya Erdogan kuundoa kivitendo mchakato huo katika vipaumbele vyake. Upande wa Ulaya pia ulisitisha mchakato huo baada ya mahakama kuwahukumu kifungo jela Selahattin Demirtaşh kiongozi wa zamani wa chama cha Kidemokrasia cha Wananchi na pia Othman Kavala. Aidha hivi sasa inaonekana hakuna upande wowote unaonyesha nia ya kufanya mazungumzo ili kujiunga Uturuki katika Umoja wa Ulaya, kutokana na sababu tofauti. Hii ni katika hali ambayo viongozi wa serikali ya Ankara wamekuwa wakikosoa mara kwa mara upuuzaji wa Umoja wa Ulaya kwa ombi la Uturuki la kupatiwa uanachama ndani ya umoja huo. Kwa kuzingatia mchakato huu wa sasa, weledi wa mambo katika eneo wanaamini kuwa, serikali ya Ankara na wananchi wa Uturuki wamenusurika na ukoloni wa Marekani na Umoja wa Ulaya. Bila lshaka wananchi wa Uturuki wana uwezo wa kujiendeshea mambo yao wenyewe na kuacha kuzitegemea serikali za Magharibi licha ya moja ya matatizo yanayoikabili nchi hiyo kutajwa kuwa ni utegemezi wake wa kiviwanda na kiuchumi kwa serikali za Magharibi.

Mwaka 1952 Uturuki ilikubaliwa kuwa mwanachama wa Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (Nato). Aidha miaka 12 iliyofuata, yaani mwaka 1964 viongozi wa Ankara waliliweka katika ajenda yao ya utekelezaji suala la kuwa miongoni mwa nchi za Ulaya. Hatua ya viongozi wa wakati huo wa Ankara ya kudhihirisha hamu ya kutaka nchi yao kuwa ya Ulaya iliungwa mkono na viongozi wa bara hilo. Pamoja na hayo, mamlaka husika za Ulaya ziliitaka Uturuki kupitisha bungune na kutekeleza nyaraka zinazohusiana na uanachama wake katika umoja huo. Kisha viongozi wa Uturuki mwaka 1987 waliwasilisha ombi rasmi la kujiunga na Umoja wa Ulaya. Lakini pamoja ya kupita miongo kadhaa hadi sasa, mazungumzo kuhusu suala hilo yamegonga mwamba. 

Aidha Ufaransa na Ujerumani zinapinga vikali Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya. Hii ni katika hali ambayo, katika uchaguzi wa karibuni wa rais wa Uturuki khususan katika duru ya pili ya uchaguzi huo uungaji mkono wa wazi wa serikali za Magharibi kwa Kemal Gulicdaroglu aliyekuwa mgombea wa muungano wa taifa wa pande sita uliandaa uwanja wa ushindi wa Recep Tayyeb Erdogan.  

Kemal Gulicdaroglu

Wanasiasa na wananchi wa Uturuki wamethibitisha kivitendo ukweli kwamba wanapinga uingiliaji wa serikali za Magharibi katika masuala ya ndani ya nchi yao, na hawawezi kuwa watekelezaji wa maagizo ya serikali za Magharibi katika eneo. Aidha tunapasa kusema kuwa: Pamoja na kupokea baadhi ya misaada ya kijeshi, bila shaka, kuendelea kwa uanachama wa Uturuki katika muungano wa Nato  pia ni kwa madhara ya serikali na watu wa nchi hiyo. Wakati huo huo, uingiliaji wa Umoja wa Ulaya katika uchaguzi wa Uturuki na jaribio la kumuondoa madarakani Erdogan umeipatia Uturuki sababu na kisingizio cha kujitenga na umoja huo. Taarifa ya pamoja ya Josep Borrell Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya na Oliver Verhli, Kamishna wa EU anayehusika na Masuala ya Ujirani na Upanuzi inaeleza kuwa umoja huo umekaribisha ushiriki mkubwa wa wananchi wa Uturuki katika uchaguzi na kudai kwamba waliwataka wananchi hao wazingatie maoni ya waangalizi wa Taasisi ya Usalama na Ushirikiano ya Ulaya na Baraza la Ulaya katika upigaji kura wao.

Jarida la Economist linalochapishwa Uingereza pia katika kukaribia duru ya kwanza ya uchaguzi wa 13 wa rais wa Uturuki liliandika bila aibu na waziwazi kuhusu uchaguzi huo kuwa: "Erdogan anapasa kuondoka, na kwa kura yako unapasa kuchukua hatua kunusuru demokrasia."   

Nalo gazeti la  Washington Post katika makaka yake iliyotiwa chumvi liliutaja uchaguzi wa Uturuki kuwa uchaguzi muhimu sana wa karne na kueleza kuwa: "Zama mpya zitaanza huko Uturuki na katika eneo baada ya kuingia madarakani Kemal Gulicdaroglu."

Misimamo kama hii ya vyombo vya habari vyenye mfungamano na serikali za Magharibi imewafanya wananchi wa Uturuki kuwa macho zaidi na njama dhidi yao. Ni wazi kuwa, Kemal Gulicdaroglu ambaye katika chunguzi zote za maoni alikuwa akiongoza mkabala wa Recep Tayyep Erdogan katika uchaguzi halisi alitanguliwa na mgombea wa muungano wa Jamhuri.

Wananchi wa Uturuki wameonyesha kuwa hawakubaliani na kuziunga mkono kibubusa  nchi za Magharibi na matakwa yao kwa sababu wanataka kujitegemea na kuwa huru. Kwa kuzingatia yote hayo , serikali ya Uturuki pia imekata tamaa na suala la kujiunga na Umoja wa Ulaya na pia Umoja wa Ulaya haujaonyesha hamu yoyote ya kuiruhusu Uturuki iliyo huru ijiunge nao pasina kufanyika nchini humo mageuzi ya kiutamaduni.

Tags