Rais wa Ukraine akataa pendekezo la amani la viongozi wa Afrika
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amepuuzilia mbali mapendekezo ya ujumbe wa viongozi wa Afrika ya kufanyika mazungumzo ya kusitisha vita na kutafuta amani ya kudumu katika eneo hilo.
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini anaongoza ujumbe wa viongozi wa Kiafrika katika jitihada za kusaka amani huko Ukraine na Russia, na baada ya kuonana na Zelensky wanatazamiwa kukutana na Rais Vladimir Putin wa Russia huko St Petersburg leo Jumamosi.
Rais wa Ukraine ameuambia ujumbe huo unaoongozwa na Ramaphosa kuwa, walipaswa kuja na mapendekezo ya jinsi ya 'kusimamisha jinai za Russia' na kutafuta njia za kuhakikisha kuwa mgogoro wa ukosefu wa usalama wa chakula unafumbuliwa.
Zelensky amesisitiza kuwa, ili kufikia makubaliano yoyote ya amani ni lazima vikosi vya Russia viondoake katika ardhi ya nchi hiyo ikiwemo katika kisiwa cha Crimea kilichodhibitiwa na Russia mwaka 2014.
Awali Ramaphosa alimuambia Zelensky kuwa, amani inaweza tu kupatikana kupitia mazungumzo, lakini Rais huyo wa Ukraine amesema mazungumzo na Russia yatawazishia maumivu Waukraine, wakati huu ambapo eti ardhi yao imekaliwa kwa mabavu.
Mbali na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, viongozi wengine walikaoambata naye huko Russia na Ukraine ni Rais Denis Sassou Nguesso wa Jamhuri ya Kongo, Abdel Fattah al Sisi wa Misri, Macky Sall wa Senegal, Hakainde Hichelema wa Zambia na Rais wa visiwa vya Comoro Azali Assoumani ambaye ni Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika (AU).
Baada ya mapuuza hayo ya Zelensky, Ramaphosa amesema, "Kwa mtazamo wetu, ni muhimu kusikiza kwa makini pande zote mbili, na sasa tutamskiza pia Rais Putin."