Ufaransa yapiga marufuku hijabu katika mashindano ya soka
Mahakama Kuu ya Utawala nchini Ufaransa imetoa kibali kwa Shirikisho la Soka la nchi hiyo cha kupiga marufuku vazi la hijabu katika mashindano ya soka ya wanawake.
Agizo hilo la Mahakama ya Utawala ya Ufaransa linasema: Shirikisho la Soka la Ufaransa linaweza kupiga marufuku uvaaji wa vazi la hijabu kwa wanawake katika mashindano ya soka, licha ya kuwa uamuzi huu unaweka mpaka wa uhuru wa kusema.
Kwa mujibu wa uamuzi huo, sasa Shirikisho la Kandanda la Ufaransa litawazuia kushiriki mashindano ya soka wanawake wanaojistiri kwa vazi la hijabu. Uamuzi huo ni kinyume kabisa na maelekezo ya Shirikisho la Soka Duniani FIFA ambalo linaruhusu wanamichezo wa mpira wa miguu kuvaa vazi la hijabu katika mashindano ya kimataifa.
Itakumbukwa kuwa, Januari mwaka jana (2022) Baraza la Seneti la Ufaransa lilipiga kura na kupasisha sheria inayopiga marufuku uvaaji wa vazi la stara na heshima la hijabu katika mashindano ya michezo.
Shirikisho la Mpira wa Miguu la Ufaransa huko nyuma limewahi kuchukua hatua za chuki dhidi ya Uislamu ambapo lilikuwa likiwakataza wanawake Waislamu kuvaa kitambaa cha kichwa katika mashindano rasmi ya michezo.
Huko nyuma pia Baraza la Seneti la Ufaransa limewahi kupasisha mpango unaopiga marufuku wasichana wenye umri chini ya miaka 18 kuvaa Hijabu katika maeneo ya umma.
Tangu Rais Emmanuel Macron aliposhika hatamu za uongozi nchini Ufaransa, vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na hata kuvunjiwa heshima matukufu ya Uislamu vimeongezeka mno katika nchi hiyo ya bara Ulaya.