Marekani inataka kutuma Ukraine mabomu 'haramu' ya vishada
Licha ya marufuku ya kimataifa ya matumizi ya mabomu ya vishada, lakini Marekani inatafakari juu ya uwezekano wa kutuma silaha hizo haramu nchini Ukraine.
Shirika la habari la CBS News limewanukuu maafisa wa Marekani ambao hawakutaka kutaja majina yao wakisema kuwa, Washington ndani ya siku chache zijazo itafikia uamuzi wa kutuma au kutotuma mabomu ya vishada nchini Ukraine.
Ripoti hiyo ya CBS News inasema kuwa, Marekani kwa sasa ipo chini ya mashinikizo makubwa kutoka Kiev, ambayo kwa miezi kadhaa sasa imekuwa ikiendesha kampeni ya kutaka kupewa silaha hizo zilizopigwa marufuku ili izitumie dhidi ya vikosi vya Russia.
Mkataba wa Kupiga Marufuku Silaha za Vishada ulianza kutekelezwa mwaka 2010, na tayari nchi zaidi ya 100 duniani zimesaini mkataba huo. Hata hivyo Marekani, Russia na Ukraine hazijasaini mkataba huo.
Haya yanajiri siku chache baada ya shirika la kutetea kaki za binadamu la Human Rights Watch kutangaza kuwa lina ushahidi mpya unaoonyesha kuwa jeshi la Ukraine linatumia mabomu ya kutega ardhini yaliyopigwa marufuku dhidi ya raia.
Human Rights Watch imeitaka serikali ya Ukraine itekeleza ahadi yake iliyoitoa mapema mwezi uliopita ya kutotumia silaha kama hizo. Vita vingali vinaendelea huko Ukraine huku nchi za Magharibi zikiendelea kuchochea moto wa vita hivyo kwa kuipatia silaha mbalimbali serikali ya nchi hiyo.