Hikma za Nahjul Balagha (25)
Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 25 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine za Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya 25.
یَا بْنَ آدَمَ، إِذَا رَأَیْتَ رَبَّکَ سُبْحَانَهُ یُتَابِعُ عَلَیْکَ نِعَمَهُ وَأَنْتَ تَعْصِیهِ فَاحْذَرْهُ
Ewe mwana wa Adam! Kila unapomuona Mwenyezi Mungu anazidi kukupa neema na wewe unaendelea kumuasi, basi jihadhari.
Kuna baadhi ya wakati, watenda maovu ambao wametenda madhambi mengi kiasi kwamba hata na wao wenyewe wanakiri kwamba madhambi yao ni mengi sana, hujidanganya kwa kufikiri kwamba Mwenyezi Mungu anawapenda na anapuuza dhambi zao licha ya makosa na uhalifu mwingi wanaoufanya. Kuna visa vkingi vimerekodiwa katika historia na vinaendelea kutokea hadi leo ambavyo vinaonesha kuweko baadhi ya watu ambao kadiri wanavyotenda dhambi, ndivyo wanavyopokea neema nyingi zaidi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa maneno mengine ni kwamba, watu hao si tu Mwenyezi Mungu hawaadhibu kwa uovu wao lakini pia anawaongezea mali, neema, umaarufu na cheo katika maisha yao hapa duniani.
Katika hikma hii ya 25 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anawaonya waovu walioghafilika na wenye kiburi kwamba kadiri wanavyoona mali na uwezo wao unaongezeka licha ya kwamba nao wanazidi kumuasi Allah, wasidhani kuwa huko ni kupendwa na Mwenyezi Mungu, bali huko ni kuzidi kupuruziwa ili wazidi kufanya maasi na adhabu yao iwe kubwa zaidi. anasema: Ewe mwana wa Adam! Kila unapomuona Mwenyezi Mungu anazidi kukupa neema na wewe unaendelea kumuasi, basi jihadhari. Naam, jihadhari sana isije ikawa huku ni kupuruziwa ili utumbukie zaidi katika maasi na adhabu kali ya Mwenyezi Mungu ikungojee.
Tutambue kuwa watendao madhambi wana daraja tofauti: baadhi yao, baada ya kufanya madhambi kiogo tu, huzinduka na kufanya haraka kutubu na kurejea kwa Muumba wao. Kundi hili hata inapotokezea kuwa na madhambi mazito zaidi, Mwenyezi Mungu huwashitua kwa njia mbalimbali na hiyo kuwa sababu ya kuzinduka na kutubu. Hiyo ndiyo inayoitwa kupendwa na Mwenyezi Mungu.
Lakini pia kuna makundi ya wanaotenda madhambi ambayo yamefikia kiwango cha juu kabisa cha uasi lakini Mwenyezi Mungu anazidi kuwaneemesha na hawashitui kwa madhambi wanayoyafanya. Watu hao huwa wanajidanganya kwa kufikiri kwamba hiyo ni ishara kuwa wanapendwa na Mwenyezi Mungu. Hivyo, wanazidi kuzama kwenye maasi, kiburi na kutojali chochote, lakini ghafla Mwenyezi Mungu huwachapa kwa mjeledi wa adhabu na kuwakamata barabara wakazama kwenye hofu na huzuni na wakashindwa kupata akili ya kurejea kwa Mola wao. Hiyo kwa hakika ndiyo adhabu chungu zaidi.
Katika kitabu cha Sharif Kafi, Imamu Sadiq AS amenukuliwa akisema: Mwenyezi Mungu anampendea kheri mja Wake, anapofanya dhambi humshitua ili akumbuke kuomba toba, na asipompenda mja Wake kutokana na matendo yake maovu, kila anapofanya madhambi mtu huo, humuongezea neema mpaka anasahau kuomba msamaha na anaendelea na maovu yake, na hivi ndivyo alivyosema Mwenyezi Mungu Mwenyewe katika surat al A'raf aya ya 182 kwamba: Na wale waliokadhibisha Ishara zetu, tutawapururia pole pole kwa namna ambayo wenyewe hawaijui.
Hapa pana swali linajitokeza nalo ni kwamba kwani kazi ya Mwenyezi Mungu si kuongoza na kuamsha, na wala si kutumbukiza watu katika mghafala na kuwafanya wakwame kwenye maasi na adhabu? Ili kujibu swali hilo tunapaswa kuzingatia ukweli kwamba taufiki ya Mwenyezi Mungu inapatikana kutokana na ustahiki na matendo ya mtu mwenyewe. Lakini kuna baadhi ya wakati watu hulewweshwa na kiburi na hujizongazonga kwenye maasi na kupoteza uwezo wote wa kusamehewa. Kwa kweli, ni matendo yao ndiyo yanayowaweka mbali na msaada na taufiki ya Mwenyezi Mungu na kuwafikisha kwenye daraja ambayo huwa hawastahili hata kuonywa, bali wanastahiki adhabu kali.