Jumapili tarehe 3 Septemba 2023
Leo ni Jumapili tarehe 17 Safar 1445 Hijria sawa na Septemba 3 mwaka 2023.
Siku kama ya leo miaka 549 iliyopita, alizaliwa Muhammad Mustafa Imad, maarufu kwa jina la Abus-Su’ud, faqihi na mfasiri wa Kiislamu katika kijiji cha Mudares karibu na mji wa Istanbul huko Uturuki. Baada ya kuhitimu masomo yake, Abus-Su’ud alijishughulisha na ufundishaji na kufanya kazi ya ukadhi mjini Istanbul, kazi aliyoendelea nayo hadi mwisho wa uhai wake. Abus-Su’ud alikuwa hodari katika masuala mbalimbali ya kijamii na aliweza kuandaa sheria za kiidara kwa mujibu wa dini ya Kiislamu katika utawala wa Othmania. Mbali na kuzungumza lugha ya Kituruki, alizungumza pia lugha za Kifarsi na Kiarabu. Msomi huyo wa Kiislamu ametunga mashairi kadhaa kwa lugha hizo. Miongoni mwa vitabu vya Abus-Su’ud ni pamoja na ‘Irshadul-Aqlis-Saliim’ ‘Dua Nameh’ ‘Qanun Nameh’ na ‘Mafrudhaat'.

Katika siku kama ya leo miaka 190 iliyopita, alizaliwa Sheikh Abdul Rahim Sultanul-Qurrai Tabrizi, qaari mkubwa wa Qur’ani Tukufu na mmoja wa walimu mashuhuri wa taaluma ya qiraa, huko mjini Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran. Baada ya kujifunza taaluma hiyo kutoka kwa baba yake, Sultanul-Qurrai Tabrizi alifahamiana na Sheikh Shamil Daghestani na kushirikiana naye. Wakati Sheikh Shamil Daghestani alipoandaa jeshi kwa ajili ya kupambana na Warusi, Sultanul-Qurrai alifanya safari kuelekea Daghestani ili kushiriki katika harakati hiyo. Baadaye alirejea Tabriz na kuanzisha chuo cha kisomo cha Qur’ani na ni wakati huo ndipo alipopewa lakabu ya Sultanul-Qurrai. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na ‘Risala katika Elimu ya Tajwidi’. Sultanul-Qurrai alifariki dunia mwaka 1336 Hijiria mjini Tabriz.
Siku kama ya leo miaka 108 iliyopita aliuawa shahidi Rais Ali Delvari, kiongozi wa mapambano dhidi ya uvamizi wa Uingereza huko kusini mwa Iran. Manzoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia vikosi vya majeshi ya Urusi kutokea kaskazini na majeshi ya Uingereza kutokea kusini viliazimia kuikalia kwa mabavu ardhi ya Iran. Wakati huo Rais Ali Delvari alitoa wito kwa wananchi kukabiliana na wavamizi wa Uingereza kwa kutegemea fatua ya vita vya jihadi iliyokuwa imetolewa na maulama wa Kiislamu ya ulazima wa kulinda nchi mbele ya maadui. Rais Ali Delvari na wapiganaji wenzake shupavu walikabiliana na mashambulizi ya mara kwa mara ya majeshi yaliyokuwa yamejizatiti kwa silaha na kuzuia kutekwa mji wa Busher. Mapambano ya wananchi wa Tengestan karibu na mji wa kuisni wma Iran wa Busher dhidi ya majeshi vamizi ya Uingereza yaliendelea kwa kipindi cha miaka 7.
Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita, Damascus mji mkongwe na wa kihistoria wa Kiislamu ulikaliwa kwa mabavu na vikosi vya majeshi ya Uingereza. Moja kati ya malengo makuu ya serikali za Ulaya wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia ilikuwa kuugawa utawala wa Othmania, lengo ambalo baadaye lilifanikiwa. Wakati utawala wa Othmania ulipokuwa ukigawanywa, maeneo yaliyokuwa chini ya utawala huo, nayo moja baada ya jingine yalidhibitiwa na Ufaransa na Uingereza, ambapo mji wa Damascus katika Syria ya leo, pia ulishambuliwa na katika siku kama ya leo ukakaliwa kwa mabavu. Hata hivyo kwa mujibu wa makubaliano ya hapo kabla kati ya London na Paris, Syria ukiwemo mji mkuu wake, Damascus, ilidhibitiwa na Ufaransa.
Miaka 84 iliyopita katika siku kama ya leo, Ufaransa na Uingereza ziliitangazia vita Ujerumani na kwa utaratibu huo Vita Vikuu vya Pili vya Dunia vikaanza. Baada ya jeshi la Ujerumani kuishambulia Poland, serikali ya Uingereza iliitumia Ujerumani ujumbe ikiitaka iondoke haraka katika maeneo inayoyakalia kwa mabavu ya Poland. Hata hivyo Ujerumani ilipuuza takwa hilo la Uingereza. Baadaye Uingereza iliipatia Ujerumani makataa ya kuhitimisha operesheni zake za kijeshi. Hata hivyo Adolph Hitler kiongozi wa wakati huo wa Ujerumani ya Kinazi alikataa kutekeleza takwa hilo. Hatimaye katika siku kama ya leo, Uingereza na Ufaransa zikaitangazia vita Ujerumani. Sio Adolph Hitler pekee ambaye hakutaraji kama Ufaransa na Uingereza zingeingia vitani kwa ajili ya Poland bali hata Joseph Stalin kiongozi wa wakati huo wa Umoja wa Kisovieti pia hakutarajia hilo.

Katika siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, mkataba wa kusalimu amri Italia katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia ulitiwa saini baina ya wawakilishi wa Italia na nchi waitifaki. Kwa mujibu wa mkataba huo, Waziri Mkuu wa Italia alikubali bila masharti kusalimu amri nchi yake na kwa utaratibu huo, mmoja wa waitifaki muhimu wa Ujerumani ya Kinazi katika vita hivyo, akawa ameondoka katika medani ya vita.
Miaka 52 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Qatar ilipata uhuru toka kwa mkoloni Mwingereza. Qatar iliwahi kudhibitiwa na Ufalme wa Othmania. Hata hivyo kufuatia kudhoofika utawala huo, Qatar ambayo kuanzia mwaka 1882 na kuendelea kivitendo ilikuwa ikiendeshwa na Uingereza, mwaka 1916 nchi hiyo ya Kiarabu ikawa imetambuliwa rasmi kuwa koloni la Muingereza. Hadi mwaka 1971 Qatar ilikuwa bado inakoloniwa na Uingereza ambapo mwaka huo huo, kwa ushirikiano wa viongozi wa eneo la pambizoni mwa kusini mwa Ghuba ya Uajemi, likaundwa Shirikisho la Umoja wa Falme za Kiarabu. Hata hivyo mnamo Septemba mwaka huo huo, yaani 1971, Qatar ilijiondoa katika Shirikisho la Umoja wa Falme za Kiarabu na kujitangazia uhuru.
Na miaka 31 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, aliaga dunia Dkt. Mahmoud Hesabi mwanafizikia mashuhuri wa Iran anayejulikana kama baba wa fizika ya kisasa ya Iran. Alizaliwa mwaka 1281 katika mji wa Tehran. Profesa Mahmoud Hesabi alikuwa na bidii kubwa masomoni na daima kuanzia masomo yake ya msingi hadi ya juu alikuwa akishika nafasi ya kwanza darasani. Sambamba na masomo shuleni, Mahmoud Hesabi alikuwa akijihusisha pia na kujifunza na kusoma dafina na hazina ya maarifa ya Kiislamu na Kiirani. Hakutoshoka na taaluma moja tu, bali alifanya hima ya kusoma fani mbalimbali. Alipofikisha umri wa miaka 17, Mahmoud Hesabi alikuwa tayari amefikia daraja za juu za masomo. Mbali na kuwa mahiri katika taaluma kama za uhandisi wa barabara, majengo, madini, umeme, fizikia na kadhalika, msomi huyu alikuwa amebobea pia katika lugha za kigeni zilizoenea duniani kama Kiarabu, Kiingereza, Kijerumani na Kifaransa. Profesa Mahmoud Hesabi aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 90 baada ya kuishi maisha yaliyojaa hima na juhudi za kielimu.