Oct 08, 2023 10:30 UTC
  • Hikma za Nahjul Balagha (32)

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Karibuni katika sehemu hii ya 32 ya mfululizo wa makala hizi fupifupi za Hikma za Nahjul Balagha. Leo pia tutaangalia kwa muhtasari hikma nyingine ya Imam Ali bin Abi Talib AS kama ilivyonukuliwa kwenye kitabu cha Nahjul Balagha tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa kipindi. Hii ni Hikma ya 32 ya mfululizo huu.

Wasikilizaji wapenzi, katika Hikma 31 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anatuelezea nguzo za imani. Suala hili la imani ni kubwa na pana sana. Ni muhimu mno kama tulivyosema kwenye kipindi kilichopita cha Hikma za Nahjul Balagha kwamba, kutokana na umuhimu mkubwa wa Imani, tumeamu kuichambua hikma hiyo ya 31 katika vipindi sita tofauti. Hii ni sehemu ya pili ya uchambuzi huo. 

Katika Hikma ya 31 ya Nahjul Balagha, Imam Ali AS anatoa tafsiri ya imani kwa upana kiasi kwamba tafsiri kama hiyo huipati kwenye kitabu kingine. Anatufundisha kuwa imani ni kitu kikubwa zaidi kuliko masuala ya kiitikadi na ni kitu ambacho kinazingatiwa pia katika masuala ya kielimu na mienendo ya watu. Ndani ya hikma hiyo amezungumzia pia hata vipengele vidogo kabisa vya kiimani na vya kiitikadi na pia vipengele vya kivitendo na kitabia ambavyo vina taathira nzuri katika kuimarisha imani ya mtu. 

Katika hikma hiyo ya 31, Imam Ali AS anatufundisha kuwa, yakini ni msingi wa pili wa imani. Yakini ni itikadi madhubuti sana ambayo inaoana na uhakika wa jambo. Kama tunavyojua, baadhi ya watu wana imani ya dini lakini hawashikamani sana na dini. Ni kama vile watu hao bado wana wasiwasi na shaka kuhusu uhakika wa dini na mafundisho yake. Ni kana kwamba yakini haijaingia katika nyoyo za watu hao.

Hapa Imam Ali anatoa ufafanuzi baada ya kusisitiza kuwa imani ina matawi manne akisema: 

فَمَنِ اشْتَاقَ إِلَى الْجَنَّةِ سَلَا عَنِ الشَّهَوَاتِ وَ مَنْ أَشْفَقَ مِنَ النَّارِ اجْتَنَبَ الْمُحَرَّمَاتِ وَ مَنْ زَهِدَ فِی الدُّنْیَا اسْتَهَانَ بِالْمُصِیبَاتِ وَ مَنِ ارْتَقَبَ الْمَوْتَ سَارَعَ [فِی] إِلَى الْخَیْرَاتِ:

Yeyote mwenye hamu ya kuingia peponi, hujiweka mbali na matamanio ya nafsi, na yeyote anayeogopa moto, hujiweka mbali na mambo ya haramu; na kila mwenye kuitaliki dunia, hayakuzi matatizo na masaibu; na yeyote aliye na yakini kuwa atakufa, hufanya haraka kutenda mema

 

Naam, Imam AS anatoa ufafanuzi wa kina ili asimbakishie mtu kisingizio cha kuacha kushikamana na imani ya kweli. Kila anayetulia na kuzingatia maneno ya kwenye hikma hii, huweza kupata ibra na kuelewa njia za kufuata ili kujiokoa katika maisha ya duniani na Akhera.

Ayatullah Makarem Shirazi, katika maelezo yake kuhusu sehemu hii ya Hikma ya 31 ya Nahj al-Balagha, anasema: Huenda elimu inayotolewa leo kwenye vyuo vikuu kuhusu Sayansi Jamii yaani matawi manne ya Sayansi Jamii huenda chimbuko lake ni matawi haya manne ya imani yaliyoelezwa hapa na Imam Ali AS. Tawi la kwanza la Sayansi ya Jamii ni elimu ya utekelezaji, la pili ni elimu ya nadharia, tatu ni elimu inayopatikana kwenye matukio yaliyopita ya historia na nne ni elimu ya nukulu ambayo inazaliwa na mila na desturi za watu. Wakati unapoyaangalia matawi hayo ya Sayansi Jamii na kuyatumia ipasavyo, bila ya shaka utaweza kufikia daraja ya yakini. Kwa mfano katika ilmu ya kumtambua Muumba, kwanza mtu anatakiwa afungue macho yake na kuangalia vizuri athari za uumbaji wa Allah duniani. Kisha anatakiwa atafakari kwa kina uhusiano wa viumbe na Muumba na hikma za kuumbwa viumbe. Baadaye apate funzo kutoka kwenye matukio ya kihistoria yaliyotokea huko nyuma na kutambua nguvu za Muumba katika matukio hayo na nne atumie hatua zilizopita kuongeza utambuzi wake na hatimaye kuwa na yakini na uwepo wa Muumba na wajibu wa kumshukuru na kumwabudu.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags