Oct 30, 2023 08:41 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Okt 30

Karibu tuangazie baadhi ya matukio ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbalimbali za dunia.

Iran yaibuka 2 Riadha ya Walemavu Hangzhou

Rais Ebrahim Raisi wa Iran ameinyooshea mkono wa pongezi timu ya taifa ya wanariadha ya Jamhuri ya Kiislamu kwa kuibuka mshindi wa pili katika mashindano ya dunia ya wanamichezo wenye ulemavu huko Hangzhou nchini China. Katika ujumbe wake huo wa tahania, Sayyid Raisi amesema: Duru ya Nne ya Michezo ya Walemavu ya Asia imekuwa ya fahari na hadhi kwa Jamhuri ya Kiislamu. Aidha amewapongeza wanamichezo wa Iran kwa kucheza kwa ari na motisha, na kuipeperusha bendera ya Iran katika mashindano hayo ya kimataifa yaliyofunga pazia lake Jumamosi ya Oktoba 28. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka ya pili kwenye mashindano hayo kwa kuzoa jumla ya medali 136.

Mamia ya wanamichezo wa Iran waling'ara kwenye mashindano hayo ya kibara katika michezo na kategoria mbalimbali na kutwaa medali 43 za dhahabu, 46 za fedha na shaba 41. Wairani wamezoa medali kochokocho kwenye michezo ya mieleka, kunyanyuauzani mzito, taekwondo na voliboli, miongoni mwa michezo mingine. Mwenyeji China imeibuka kidedea kwenye mashindano hayo kwa kuzoa zaidi ya medali 500, zikiwemo dhahabu zaidi ya 200. Orodha ya tatu bora imefungwa na Japan, huku nafasi ya nne na tano zikitwaliwa na Korea Kusini na India kwa usanjari huo. Haya ndiyo matokeo bora zaidi kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika historia ya Michezo ya Walemavu ya Asia.  Mapema mwezi huu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilimaliza katika nafasi ya saba kwenye Michezo ya Asia iliyofanyika huko Hangzhou nchini China, baada ya kukusanya jumla ya medali 54 kwenye mashindano hayo.  

Kombe la Dunia Raga: Afrika Kusini bingwa

Afrika Kusini imetwaa Kombe la Dunia kwenye mchezo wa raga kwa mara ya nne sasa, baada ya kuisasambua New Zealand michapo 12-11 katika mchezo wa fainali ya mwaka huu uliopigwa Jumamosi. Hadre Pollard aliifungia Afrika Kusini mipigo minne ya penati kwenye fainali hiyo iliyochezewa katika Uwanja wa Taifa wa Ufaransa eneo la Saint-Denis, viungani mwa Paris, mji mkuu wa Ufaransa.  

Timu ya raga ya Afrika Kusini

Nyota wa tenisi duniani, Roger Federer na Novak Djokovic ni miongoni mwa mashabiki zaidi ya elfu 80 waliokuwa uwanjani hapo kushuhudia fainali hiyo ya kukata na shoka. Mchezaji bora wa mechi, Pieter-Steph du Toit amesema: Michezo mitatu iliyopita tumekuwa na wakati mgumu. Kama timu tunapenda vimbwanga. Tunaona fahari kucheza kwa niaba ya taifa zima la Afrika Kusini na Springboks. Tunatazamia kupata mapokezi ya kukata na shoka nyumbani. Springboks kabla kubebe taji la mwaka huu 2023, walitwaa kombe la dunia la raga mwaka 1995, 2007 na 2019.

Ligi ya Soka Afrika

Wawakilishi wa Tanzania katika Michuano ya African Football League, klabu ya Simba SC imetupwa nje ya michuano hiyo baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Ahly nchini Misri. Mchezo huo wa robo fainali mkondo wa pili ulipigwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Cairo na kuishuhudia Ahly ikivuka hatua ya nusu fainali kwa faida ya magoli mengi ya ugenini baada ya kutoka sare ya magoli 2-2 kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza. Katika mchezo wa marudiano, Simba walijikuta muda mwingi wa mchezo wakizuia baada ya Al Ahly kuonekana kuingia katika mchezo huo wakisaka ushindi tangu dakika ya kwanza ya mchezo. Goli la Simba lilifungwa na Sadio Kanoute kunako dakika ya 67 ya mchezo kabla ya Ahly kusawazisha katika dakika ya 75 kupitia kwa Mahamoud Kahraba. Licha ya Simba kuwa na vizingiti vya kutinga hatua ya nusu fainali katika michuano ya kimataifa, uongozi wa klabu hiyo umewapongeza wachezaji namna walivyopambana ugenini na kutoka sare ya bao 1-1. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema walitolewa kimchezo, lakini wao kama viongozi hawana deni na mastaa wao kutokana na ubora waliouonyesha.

Nembo ya Shirikisho la Soka Afrika CAF

Wakati huohuo, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini imeifuata Al Ahly kwenye hatua ya nusu fainali ya Kombe la Afrika (AFL) kufuatia ushindi wa jumla wa 2-0 dhidi ya vigogo wa Angola, Petro de Atletico. Waafrika Kusini hao walivuna vinono kwenye mchuano wa mkondo wa kwanza, kabla ya kulazimishwa sare tasa na Waarabuu kwenye mechi ya mkondo wa pili. Nayo klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imesukumizwa nje ya michuano hiyo ya African Football League kufuatia kipigo cha jumla cha mabao 3-1 dhidi ya vigogo wa Tunisia, Esperance de Tunis. Mazembe ilishinda goli 1-0 katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa katika dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar, kabla ya kukubali kichapo cha magoli 3-0 ugenini katika dimba la Olympique Hammadi Agrebi mjini Rades, Tunisia. Esperance imetangulia nusu fainali kucheza na Wydad Casablanca. Casablanca hiyo ilitinga hatua ya nusu fainali kufuatia ushindi wa jumla wa 4-0 dhidi ya miamba ya Nigeria, Enyimba FC katika dimba la Mohamed wa 5 mjini Casablanca. Wydad ilishinda 1-0 katika mchezo wa mkondo wa kwanza huko Nigeria kabla ya kushusha kipondo cha 3-0 nyumbani na kuifuata Esperance ya Tunisia kwenye nusu fainali.

Mpira wa magongo; Kenya yaizima Zambia

Timu ya taifa ya mpira wa magongo ya wanawake ya Kenya imeanza vyema kampeni ya kusaka tiketi ya kushiriki Michezo ya Olimpiki ya Paris mwaka ujao 2024, kwa kuibamiza Zambia alama 4-0. Akina dada hao wa Kenya waling'ara kwenye mechi yao hiyo ya ufunguzi ya Kundi B iliyopigwa mjini Pretoria nchini Afrika. Kenya ipo Kundi B pamoja na Ghana, Namibia na Zambia. Kundi A ina miamba kama Nigeria, Afrika Kusini na Zimbabwe. Nayo Crested Cranes ya Uganda iliiadhibu Cameroon mabao 2-0 katika mechi yake. Washindi wa michuano hiyo ya kufuzu kwa upande wa Afrika, watajiunga na Ufaransa, Australia, Uholanzi, India, na China kupata tiketi ya moja kwa moja ya kushiriki Michezo ya Olimpiki ya Paris itakayotifua mavumbi mwaka ujao nchini Ufaransa.

Dondoo za Hapa na Pale

Katika Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, kinda Eddie Nketiah alifunga hatrick yake ya kwanza Jumamosi wakati Arsenal iliichabanga Sheffield United mabao 5-0 nyumbani Emirates. Wabeba Bunduki waliutandaza mpira na kuwapeleka mchakamchaka mahasimu wao katika takriban kipindi chote. Mbali na mabao matatu yaliyofungwa na Nketiah, bamdogo huyo mwenye umri wa miaka 24 pekee, Gunners waliliyumbisha na kulizamisha kabisa jahazi la Sheff United kwa mabao ya Fabio Vieira na Takehiro Tomiyasu. Ushindi huo umeifanya Arsenali iwe na mwanya wa pointi 2 nyuma ya mahasimu wao wa London Kaskazini, klabu ya Tottenham ambayo ipo kileleni mwa jedwali kwa alama 26. Siku ya Jumapili, watani wa jadi, Manchester United na Manchester City walivaana katika debi la Manchester lililopigwa katika Uwanja wa Old Trafford. Licha ya kuupigia nyumbani, lakini Mashetani Wekundu walilishwa kichapo cha mbwa cha mabao 3-0. Nyota Erling Halaand aliifungia City mawili katika dakika za 26 na 49, kabla ya kumuandalia mazingira Phil Foden ambaye aliwatuma kuzimu Devils katika dakika ya 80 ya mchezo.

Kabla ya hapo, Liverpool iliipa kichapo kikali Nottingham Forest, kinachofanana na dozi iliyopokea United. Aidha Chelsea ilishukiwa vibaya na Brentford katika mchuano mwingine wa EPL, huku mabao ya Ethan Pinnock na Bryan Mbeumo yakitosha kuwadhalilisha The Blues.

Na mchezaji nyota wa soka Cristiano Ronaldo aliifungia klabu yake ya al-Nassr ya Saudi Arabia mabao mawili katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Asia dhidi ya al-Duhail ya Qatar, ambao uliishia kwa Wasaudia kuibuka na ushindi wa mabao 4-3. Aidha alimpa pasi ya kiufundi kwa kutumia kisigoni, Anderson Talisca aliyefanikiwa kuwafunga pia al-Duhail. Bao jingine la Nassr kwenye mchuano huo lilitiwa kimyani na Sadio Mane.

………………….TAMATI…..………..