Tebboune: Tunao ushahidi unaothibitisha ukatili wa jinai za kikoloni za Ufaransa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136686-tebboune_tunao_ushahidi_unaothibitisha_ukatili_wa_jinai_za_kikoloni_za_ufaransa
Rais wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune, ametangaza kwamba nchi yake iko tayari kuwasilisha nyaraka, ushahidi na ushuhuda kwa vyombo vya kisheria vya Afrika ambavyo "vinathibitisha uhalifu mbaya" wa ukoloni wa Ufaransa nchini Algeria.
(last modified 2026-02-16T05:59:35+00:00 )
Feb 16, 2026 05:59 UTC
  • Abdelmadjid Tebboune
    Abdelmadjid Tebboune

Rais wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune, ametangaza kwamba nchi yake iko tayari kuwasilisha nyaraka, ushahidi na ushuhuda kwa vyombo vya kisheria vya Afrika ambavyo "vinathibitisha uhalifu mbaya" wa ukoloni wa Ufaransa nchini Algeria.

Haya yamekuja katika hotuba ya Tebboune kuhusu utafiti ulioandaliwa na Kamati ya Kisheria ya Umoja wa Afrika, ambao umewasilishwa kando ya Mkutano wa 39 wa AU uliofanyika Februari 14 na 15 katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.

Utafiti huo unaorodhesha ukoloni wa Ufaransa kama "uhalifu dhidi ya ubinadamu," na unatambua baadhi ya vitendo vilivyofanywa wakati wa utumwa na kuhamishwa watu kwa mabavu kama "vitendo vya mauaji ya kimbari" dhidi ya watu wa Afrika. Utafiti huo pia unaangazia athari za kisheria za hatua hiyo.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri Mkuu Sifi Gharib, Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria, amesema kwamba nyaraka za kihistoria zilizoko mikononi mwa Algeria zinaonyesha ukatili na ukiukwaji mkubwa wa sheria uliofanywa ili kukandamiza "mapambano ya watu wa Algeria," ikiwa ni pamoja na utumiaji wa njia na mbinu zilizopigwa marufuku chini ya sheria ya kimataifa.

Tebboune amesema kwamba Bunge la Algeria lilipiga kura kwa kauli moja - mnamo Desemba 24, 2025 - na kupasisha sheria inayotambua ukoloni uliofanyika nchini Algeria kuwa ni kosa la jinai.

Sheria hiyo inaitaka Ufaransa kuomba msamaha na kutoa fidia kwa watu wa Algeria. Vilevile inajinaisha hatua yoyote ya kusifu ukoloni, ikilaani "jinai za kipindi cha ukoloni wa Ufaransa," ikiwa ni pamoja na "mauaji nje ya mfumo wa mahakama, mateso, ubakaji, majaribio ya silaha za nyuklia (katika ardhi ya Algeria) na uporaji wa kimfumo wa rasilimali za nchi hiyo."

Rais wa Algeria ameeleza tena uungaji mkono kamili wa nchi yake kwa mipango yote inayofanywa na Tume ya Umoja wa Afrika inayolenga kuanzisha mbinu ya kisheria iliyo wazi ambayo inaorodhesha ukoloni wa Ufaransa katika nchi za Afrika kuwa ni miongoni mwa uhalifu mkubwa zaidi wa kimataifa.

Katika kikao chao cha 39 cha kawaida kilichofanyika Jumapili jijini Addis Ababa, Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) walipitisha “Azimio la Algiers” kuhusu uhalifu wa kikoloni barani Afrika.

Viongozi wa Afrika pia waliamua kuitambua tarehe 30 Novemba kama siku ya kuwakumbuka mashahidi na waathiriwa wa biashara ya utumwa ya kuvuka Atlantiki, ukoloni, na mfumo wa ubaguzi wa rangi (apartheid), wakisisitiza kuwa kumbukumbu ya pamoja ni msingi muhimu wa utambuzi wa haki, kupatikana kwa uadilifu, na kuzuia kurudia kwa uhalifu kama hiyo katika siku zijazo.

Azimio la Algiers linazitaka nchi zilizokuwa tawala za kikoloni “kubeba kikamilifu wajibu wao wa kihistoria kwa kutambua hadharani na kwa uwazi dhulma zilizofanywa na wakoloni hao.”